
Chama cha ACT Wazalendo kupitia jimbo la Ndanda kimemuidhinisha Ndugu Cecil Francis Akili kuwa mtia nia wa ubunge kwa uchaguzi mkuu ujao.
Ndugu Akili ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho katika jimbo hilo na Katibu wa Mipango na Uchaguzi kwa Mkoa wa Mtwara, amethibitisha kuwa atachukua fomu rasmi ya kugombea nafasi hiyo tarehe 14 Agosti, mara muda wa kiserikali utakapowadia.
Akizungumza na wanahabari, Ndugu Akili amesema kuwa uamuzi wake wa kutangaza nia ya kugombea umetokana na hali ya maendeleo ya jimbo hilo, ambayo amedai haiendani na matarajio ya wananchi.
Ameeleza kuwa amejitathmini na kuona ana uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa kuwashika mkono katika safari ya mabadiliko kupitia itikadi na dira ya ACT Wazalendo.
Aidha, Ndugu Akili ameeleza kuwa uteuzi wake na chama unatokana na imani waliyo nayo kwake baada ya tathmini ya kina kufanyika.
Amesisitiza kuwa hana budi kuomba ridhaa kwa wananchi wa Ndanda kwa ajili ya kuwaongoza katika hatua muhimu ya maendeleo, huku akiwataka wanachama na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono katika safari hii ya kisiasa.
Akili ameahidi kuwa, endapo atapata ridhaa hiyo, atatekeleza kwa uaminifu ilani ya ACT Wazalendo, hasa katika vipengele vyote 36 vya chama hicho.
Ametaja maeneo ya huduma bora za afya, elimu bora, na miundombinu madhubuti kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vyake atakavyoshughulikia mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Ndanda.