Wachimbaji 25 katika mgodi mdogo wa dhahabu unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, uliopo Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga mkoani Shinyanga, wamefukiwa na kifusi baada ya mgodi huo kutitia wakati zoezi la ukarabati wa maduara likiendelea.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, inaendelea na zoezi la uokozi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wachimbaji wenzao.
Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa ni kutitia kwa ardhi wakati shughuli ya matengenezo ya maduara ikiendelea.
Hadi sasa zoezi la uokozi limefanikiwa kwa kuokolewa watu watatu kati ya 25 waliofukiwa kwenye mgodi huo.
Jitihada za kuwaokoa wengine zinaendelea chini ya usimamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.