Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa limeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kutoa msaada wa mashuka 250, yenye thamani ya Shilingi Milioni 5.3 na kushiriki zoezi la uchangiaji damu katika hospitali nne za mkoa huo.
Zoezi hilo limefanyika Oktoba 7, 2025, katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Hospitali ya Halmashauri ya Msalala, Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na Hospitali ya Manispaa ya Kahama, likiwa na lengo la kutoa huduma kwa jamii na kuonesha mshikamano wa shirika hilo na wananchi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Bi Emma Nyaki, amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazotekelezwa na shirika hilo kila mwaka wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja Duniani.
“Tumejipanga kuhakikisha huduma bora kwa wateja zinakwenda sambamba na kuchangia ustawi wa jamii. Tunatoa mashuka 40 kwa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, 40 kwa Hospitali ya Msalala, 40 kwa Ushetu, 50 kwa Hospitali ya Manispaa ya Kahama, na 60 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga,” amesema Nyaki.
Ameongeza kuwa, mbali na misaada hiyo, watumishi wa TANESCO wamejitolea kushiriki katika uchangiaji wa damu salama, ili kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo katika hospitali za mkoa huo.
Aidha, viongozi wa hospitali zilizopokea msaada huo wameishukuru TANESCO kwa moyo wa kujitolea na kuendelea kuwa karibu na jamii, wakisema kuwa mashuka hayo na damu salama vitasaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka duniani kote kwa lengo la kuimarisha mahusiano kati ya watoa huduma na wateja wao.