
Na Sumai Salum-Kishapu
Wananchi wa Kijiji cha Unyanyembe Kata ya uchunga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wamepongeza juhudi za Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Lucas Manyegule, kwa kushirikiana nao kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji baada ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya Tsh. Milioni 2.35 vikiwemo kompyuta ya mezani (desktop) na printa, kwa Shule ya Awali na Msingi Uchunga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 24, 2026 wenye lengo la kukabidhi na kusomewa mapato na matumizi ya fedha hiyo, wananchi hao wamesema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwa kuwa inaonesha dhamira ya Diwani huyo ya kuwatumikia wananchi na kuchochea maendeleo ya elimu. wamesema ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni muhimu katika kutatua changamoto zinazozikabili shule na kuboresha huduma kwa jamii.
Kwa upande wake, Patrick Said, mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, amemshukuru Mhe. Diwani Manyegule kwa msaada huo na wananchi wote waliohusika, akieleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia walimu kuandaa na kuchapisha mitihani kwa urahisi, kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuongeza ari ya wanafunzi kusoma na kufanya vizuri katika mitihani yao.
“Hapo kabla tulikuwa tunapeleka fedha shuleni kwa ajili ya kuchangia kuchapisha mitihani na wakati mwingine tulikuwa tunaandikiwa ubaoni na kisha tunanakili kwenye makaratasi ila kwa sasa uwepo wa mashine hizo unatufanya na sisi tujione tunathaminika” Ameongea Mwanafunzi Grolia Mtalimwa.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Mwl. Neema Alex Shayo, amesema vifaa hivyo vitaboresha maandalizi, uchapishaji na utoaji wa mitihani, pamoja na kuongeza ufanisi wa kazi za walimu. Amesema changamoto ya kukosekana kwa kompyuta na printa ilikuwa imewasilishwa tangu Septemba mwaka jana kwa Diwani wakati akiwa ndiye mgeni rasmi katika mahafali yaliyofanyika shuleni hapo na sasa kwa niaba ya Walimu wa shule hiyo wnaanshukuru kw akulibeba na sasa kulitekeleza huku wakiahidi kuinua matokeo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Diwani wa Kata hiyo Mhe. Lucas Manyegule amewapongeza wananchi, walimu na wadau wa maendeleo waliochangia fedha na kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo. Amesema maendeleo yanahitaji ushirikiano wa pamoja na kwamba ataendelea kushirikiana na wananchi kutatua changamoto zilizopo, huku akilenga kuona Vijiji vya Unyanyembe, Ngundangali na Kakola vinanufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Walipowasilisha hitaji lao niliumia sana kuona walimu wakienda Shinyanga mjini au Mhunze kwa ajili ya kuchapisha mitihani nikaamua kuwashirikisha wanafunzi wenzangu tuliosomea shuleni hapa na baadae wananchi tulipowashirikisha kiukweli mlionesha utayari nawashukuru sana hakika kwa mchango wenu wa 852,000 jumla nilikusanya na sasa imebakia 4,22,000 hiyo pia tutaendelea kupunguza changamoto zingine shuleni hapo” Ameongeza Mhe. Manyegule
Juhudi hizo zinaonesha namna madiwani wa Wilaya ya Kishapu wanavyojitolea na kuwashirikisha wananchi katika kuleta maendeleo na kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, hususan katika sekta za elimu, afya na lishe, kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.
