
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Usimamizi wa Ziwa Tanganyika kuimarisha utekelezaji wa maamuzi na mikakati ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinanufaisha jamii za nchi zinazolizunguka.
Alisema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu ya kiikolojia na kiuchumi inayotegemewa na zaidi ya watu milioni 13 katika nchi nne zinazopakana nalo, kupitia shughuli za uvuvi, usafirishaji wa watu na bidhaa na uhifadhi wa viumbehai.
Muyungi alisema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 15 wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), uliofanyika Oktoba 25, 2025 jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa maamuzi ya mkutano huo yanapaswa kutafsiriwa katika hatua zinazotekelezeka na kuimarisha usimamizi wa ziwa na rasilimali zake.
Alitaja changamoto zinazokabili bonde hilo kuwa ni athari za mabadiliko ya tabianchi, mbinu za uvuvi zisizo endelevu na uchafuzi wa mazingira katika baadhi ya maeneo na kusema hali hiyo inaathiri mifumo ya ikolojia na fursa za uchumi wa bluu.
Alisema nchi wanachama zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mkataba, ikiwemo kulipa michango ya kifedha kwa wakati na kutekeleza maamuzi ya mikutano ya mawaziri, mipango kazi na bajeti zilizoainishwa.
Aidha, alizitaka nchi wanachama na sekretarieti ya mamlaka hiyo kuimarisha uwezo wa kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili kutoka mifuko ya kimataifa, ikiwemo Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (Global Environment Facility).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Mfumu Richard alisema ziwa hilo ni rasilimali muhimu kwa nchi wanachama kutokana na mchango wake katika upatikanaji wa maji, uvuvi, bayoanuwai na shughuli za kiuchumi.
Alisema pamoja na umuhimu wake, ziwa hilo linakabiliwa na changamoto zinazoongezeka, zikiwemo uvuvi usio endelevu, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa makazi ya viumbehai, athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu.
Alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza rasilimali za kifedha kwa ajili ya usimamizi na ulinzi wa ziwa hilo ili liendelee kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, na Mwenyekiti wa wajumbe (LTA) Tanzania, Kemilembe Mutasa, alisema Ziwa Tanganyika si mpaka wa kijiografia, bali ni rasilimali muhimu inayozileta pamoja nchi hizo kutokana na mchango wake katika maisha, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.
Alisema maamuzi na ushauri wa Kamati ya Usimamizi kwa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika ni muhimu katika kuhakikisha mamlaka hiyo inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dkt. Emma Liwenga, alisema mamlaka hiyo inaangalia njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto za mazingira zinazolikabili ziwa, ikiwemo uchafuzi, athari za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa samaki.
Dkt. Liwenga alisema Ziwa Tanganyika lina fursa nyingi za kiuchumi zinazotokana na uvuvi, utalii na usafirishaji, hivyo ni muhimu kuhakikisha rasilimali zake zinasimamiwa kwa njia endelevu kwa manufaa ya jamii zinazozunguka bonde hilo.
