
Kampeni ya Ongea na Kamanda imeendelea katika Kata ya Maganzo, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amekutana na wananchi na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, kuimarisha malezi bora ya watoto na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika masuala ya usalama.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano huo leo Oktoba 28,2026, Kamanda Magomi aliwapongeza kwa umoja na mwitikio wao wa kushiriki katika kampeni hiyo, akieleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kuimarisha usalama na kudumisha amani katika jamii.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu, akiwataka wananchi kujiepusha na vikundi vinavyoweza kuhatarisha usalama, huku akibainisha kuwa mazingira yenye amani ni msingi wa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Katika suala la malezi, Kamanda Magomi aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanalelewa katika maadili mema yanayozingatia utamaduni wa Mtanzania. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwapeleka watoto katika nyumba za ibada ili kuwajengea misingi ya kiroho na maadili yatakayowasaidia kukua wakiwa na heshima, nidhamu na uwajibikaji.
Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Sungusungu katika kata hiyo na kuahidi kuchangia matofali 1,000 ili kusaidia kukamilika kwa mradi huo. Aidha, alikubali ombi la viongozi wa Sungusungu la kuwa msimamizi wa jengo hilo, hatua inayolenga kuunga mkono juhudi za jamii katika kuimarisha shughuli za ulinzi shirikishi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu, Mrakibu wa Polisi Ester Gesogwe, alikabidhi mifuko 16 ya saruji ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyokuwa ametoa awali kwa ajili ya ujenzi huo. Alisema mchango huo si wa mwisho, akiahidi kuwa ataendelea kusaidia hadi jengo hilo litakapokamilika.
Wananchi wa Kata ya Maganzo waliishukuru Jeshi la Polisi kwa michango na ushirikiano wake katika kusaidia ujenzi wa jengo hilo. Pia waliahidi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kulinda amani, kuimarisha usalama na kuzuia vitendo vya uhalifu katika eneo lao.
Kampeni ya Ongea na Kamanda inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, kutoa elimu ya usalama na kujenga ushirikiano wa pamoja katika kuzuia uhalifu na kudumisha amani katika jamii.
