
Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba SC imesema imesikitishwa na kauli zilizotolewa hadharani na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa Novemba 15, 2026, Simba imeeleza kuwa Novemba 13, mwaka huu, iliwasilisha barua rasmi kwa TFF ikieleza msimamo wake kuhusu mwenendo wa mchakato wa uchaguzi, pamoja na kutoa mapendekezo ya maboresho na kuomba majibu rasmi kwa maandishi.
Hata hivyo, Bodi hiyo imehoji uamuzi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kujibu hoja hizo kupitia vyombo vya habari kabla ya kuipatia klabu majibu rasmi kwa maandishi, ikieleza kuwa hatua hiyo haizingatii utaratibu unaostahili.
Aidha, Simba imekanusha vikali maelezo yanayoashiria kuwa klabu hiyo ina makundi mawili yanayokinzana, yakihusishwa na ofisi ya mwekezaji iliyopo Masaki na ofisi ya Mzee Mangungu iliyopo Msimbazi.
Klabu hiyo imesisitiza kuwa Simba ni taasisi moja yenye katiba moja inayopaswa kuheshimiwa na kufuatwa na viongozi, wanachama pamoja na wadau wake wote.
Imefafanua kuwa katiba inayotumika ni toleo la mwaka 2018 lililofanyiwa marekebisho Novemba 30, 2025 na kusajiliwa rasmi Februari 18, 2026.
Katika taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi imesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa uhuru, haki, uwazi na uaminifu, kwa kuzingatia katiba ya klabu, kanuni za uchaguzi pamoja na kanuni za TFF na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Wakati huo huo, Simba imeeleza kuwa jopo lake la wanasheria linaendelea kupitia na kutathmini hatua zaidi za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Pamoja na msimamo huo, Bodi imewaomba wanachama, mashabiki na wadau wa klabu hiyo kuwa watulivu, kuepuka migawanyiko na kuendelea kudumisha umoja wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea.


