
Chama tawala nchini Senegal, PASTEF, kimetangaza kumfukuza uanachama Rais wa nchi hiyo, Bassirou Diomaye Faye, pamoja na wanachama wengine 31 kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Reuters na Africanews, uamuzi huo ulifikiwa kati ya Novemba 17 na 18, 2026, baada ya chama hicho kubaini kuwa baadhi ya wanachama hao walikuwa wameanzisha au kujiunga na chama kingine cha kisiasa, hatua inayokiuka masharti ya uanachama wa PASTEF.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo uhusiano wa kisiasa kati ya Faye na Ousmane Sonko, ambaye ni mmoja wa viongozi wakuu wa chama hicho na Waziri Mkuu wa Senegal, umeendelea kuzorota kutokana na tofauti za kisiasa na namna ya kuendesha Serikali.
Mgogoro huo umeibua maswali kuhusu mustakabali wa Serikali ya Senegal, hasa kutokana na nguvu kubwa ya PASTEF ndani ya Bunge, ambako ina wabunge 130 kati ya 165, huku chama kipya cha Faye kikiwa hakina uwakilishi wowote bungeni.
Hali hiyo inaweza kuongeza changamoto katika kupitisha bajeti na kutekeleza mipango ya kiuchumi, pamoja na juhudi za Senegal kupata msaada wa kifedha kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Pamoja na kufukuzwa kwake ndani ya PASTEF, Faye bado anaendelea kushikilia nafasi ya Rais wa Senegal, huku mgogoro huo ukiashiria mpasuko mkubwa wa kisiasa kati ya viongozi wawili waliowahi kuwa washirika wa karibu.
