
Na Nyamiti A. Nyamiti
Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imeanza rasmi zoezi la kuwajengea uwezo wataalam wa Kata kuhusu uibuaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia mfumo mpya ulioboreshwa wa O&OD, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2027/2028.

Mafunzo hayo yalizinduliwa Novemba 18 katika Kata ya Malunga na yanaendeshwa na Maafisa Mipango kutoka Manispaa ya Kahama. Lengo kuu ni kuhakikisha wataalam wa Kata wanapata uelewa wa kutosha ili waweze kushusha elimu hiyo hadi ngazi za Vijiji na Mitaa, na hivyo kuwawezesha wananchi wenyewe kupendekeza miradi inayoakisi mahitaji yao ya kimaendeleo.

Afisa Mipango wa Manispaa, William Maziku, aliyekuwa akizungumza wakati wa mafunzo hayo, aliwasisitiza viongozi wa Kata kuhakikisha wanauelewa mfumo huo mpya ili wawe mabalozi wazuri kwa wananchi katika kubaini changamoto zao na kuzigeuza kuwa maandiko ya miradi.
Maziku aliongeza kuwa kushirikisha wananchi tangu hatua za awali ni msingi wa kupata miradi bora inayogusa maisha ya watu na kuleta maendeleo yenye tija.

Mafunzo hayo pia yanatolewa na wakufunzi wengine kutoka Manispaa, akiwemo John Modest na Edina Malegesi.
Kwa mujibu wa ratiba, zoezi hili litatekelezwa katika Kata zote 20 zinazounda Manispaa ya Kahama, ambapo wananchi watapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uandaaji wa Mpango na Bajeti ya 2027/2028.

