Kauli ya ‘ndiyo’ ya spika mstaafu, Job Ndugai wakati wa kupigia kura bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024 iliamsha shangwe bungeni wakati wa upigaji wa kura wa bajeti hiyo leo.
Wabunge walianza kupiga kura saa 5:30 asubuhi baada ya hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba.
Katika zoezi hilo lililotanguliwa na mwongozo wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akinukuu ibara ya 90 (2) (b), wabunge walipiga kura ya wazi kwa kila mmoja kuitwa jina lake na kujibu ndiyo kwa wanaokubali na wengine wachache kuitikia ‘abstain’ (hawakubali wala hawakatai) akiwemo Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.
Katika zoezi hilo, Ndugai alikuwa mtu wa tatu kutajwa kupiga kura, akitanguliwa na Naibu Spika Mussa Zungu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Baada ya Ndugai kutamka ndiyo, Spika Tulia alitoa maelekezo mafupi ya kuwasha spika katika zoezi hilo, kisha Ndugai akatajwa tena ili kurudia kupiga kura na kumtaka ndiyo huku akipigiwa makofi mengi na wabunge ukumbini hapo.