
Israel na Iran zimeendelea kushambuliana huku Israel ikianza kurudisha nyumbani raia walioko nje. Kwingineko, Marekani imeufunga kwa muda ubalozi wake ulioko Jerusalem hadi Ijumaa. China imeanza kuondoa raia wake Iran.
Mapema Jumatano, milipuko ilisikika mjini Tehran, kufuatia mashambulizi makali ya angani yanayofanywa na Israel, yakiulenga mji huo mkuu wa Iran.
Jeshi la Israel (IDF) lilitangaza kushambulia Tehran. Kwenye akaunti yake ya Telegram jeshi hilo limesema limeshambulia kituo cha urutubishaji urani na vituo vingine kadhaa vya kutengeneza silaha vinavyomilikiwa na utawala wa Iran.
Baadaye, IDF iliripoti kuwa imegundua makombora kutoka Iran yanayoelekea Israel tena, na kwamba Jeshi la Anga la Israel linafanya operesheni ya kuondoa tishio hilo.
Brigedia Jenerali Effie Defrin, msemaji wa jeshi la Israel amesema “tunalenga vituo vya kijeshi, wao wanashambulia nyumba za raia. IDF itaendelea kufanya operesheni kwa usahihi, kw anguvu na kwa uthabiti ili kuhakikisha usalama wa watu wa Israel.”
Mapema, Jumatano, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmail Baghaei, akihojiwa na kituo cha televisheni ya Aljazeera, alitoa tahadhari kwamba uingiliaji wa Marekani katika mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya nchi yake, unaweza kuchochea ‘vita kamili’.
Iran yadai kudhibiti mifumo ya ulinzi wa angani ya Israel
Walinzi wa Mapinduzi wa Iran wamedai kufanya wimbi la 11 la makombora dhidi ya Israel. Wamesema mashambulizi hayo yanaashiria mwanzo wa mwisho wa mifumo ya ulinzi ya angani ya Israel.
Msemaji wa jeshi hilo Iman Tajik amesema Iran imetumia makombora ya Fattah aliyodai yalishinda mifumo ya ulinzi ya Israel, na kutaja tukio hilo kuwa ujumbe kwa Marekani.
