Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kugombea tena nafasi ya ubunge wa viti maalum kwa wanawake kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Fomu hiyo imekabidhiwa kwa Makamba Jumapili, Juni 29, 2025 na Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Shinyanga, Bi. Habiba Musimu, katika ofisi za chama mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Salome Makamba amesema kuwa endapo atapewa ridhaa na chama, ataendelea kuwatumikia na kuwasemea wanawake wa Mkoa wa Shinyanga kwa moyo wa uzalendo, bidii na uaminifu mkubwa.
“Nina uzoefu, dhamira ya kweli na moyo wa kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake. Niko tayari kuendelea kuwatumikia kwa heshima kubwa,” amesema Makamba.