Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya Wananchi wa Kata ya Majengo iliyopo Mtaa wa Sokola Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wanadaiwa kutupa taka ngumu kwenye makaburi baada ya Kampuni yenye tenda ya Kukusanya taka kumaliza mkataba katika eneo hilo.
Makaburi ya Sokola manispaa ya Kahama ni ya muda mrefu ambayo zamani yalikuwa nje ya Mji, ila kutokana na kasi ya Maendeleo kwa sasa yapo Katikati ya Makazi ya watu katika Kata ya Majengo, yakitazamana na Shule ya Msingi Majengo.
Baadhi ya wananchi wa Kahama ambao wamezika ndugu zao katika makaburi hayo, wamelalamika kitendo hicho cha kukuta uchafu katika eneo hilo, huku wakiiomba serikali kuweka uzio ili kudhibiti hali hiyo.
“Kwa kweli inasikitisha sana, kila siku tunakuta uchafu kwenye makaburi kama mimi Babu yangu tumemzika hapa mara ukute maganga ya ndizi, viazi wakati mwingine hata pampas na taulo za kike zilizotumika kwakweli inauma sana hasa sisi wenye ndugu hapa,” alisema Gladess Maiko.
Aidha, wameomba eneo la makaburi liwekewe uzio, ili kuzuia watu wanaoingia na kutupa taka eneo hilo sambamba na kuepuka wizi wa misalaba na vigae unaofanywa na watu wasiofahamika.
“Tatizo la Hapa siyo taka tu bali hata wizi wa misalaba kwa ajili ya vyuma chakavu, watu wanaiba misalaba na wengine wanabandua hadi vigae vilivyojengewa kaburi kwa hiyo tunaomba serikali wajenge hata uzio ili kuzuia hali hii maana eneo la makaburi ni eneo la Ibada linapaswa kuheshiwa,” amesema Gidion James Mkazi wa Shunu Kahama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, Patroba Ndabigeze amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa chanzo ni kukosekana kwa gari ya kuzoa taka katika mtaa huo hali ambayo baadhi ya wananchi wameona kigezo cha kutupa taka eneo la makaburi.
“Hili tatizo lipo na wananchi wanatupa uchafu kwa siri nyakati za usiku,wanafanya hivi baada ya kukosekana kwa Magari ya kuzoa taka katika mtaa wetu tumeweka doria ila hakuna tuliyemkamata na hata kama ukimkamata akiuliza magari utajibu nini,kwahiyo hili swala linasababishwa na kukosekana kwa magari,” amesema Ndabigeze.
Kwa upande wake Afisa kutoka Kampuni ya Gin Investment ambao wamepewa uzabuni wa kuzoa taka manispaa ya Kahama ambaye hakutaka jina lake lifahamike kwa sababu siyo msemaji wa Kampuni amesema kuwa kampuni yao ilishamaliza mkataba na serikali tangu Mwezi July na kwamba kwa sasa eneo la Majengo Sokola halina Mzabuni.
“Toka mwezi wa saba kampuni yetu ilimaliza mkataba na serikali, ila zamani tulikuwa tunazoa taka hadi maeneo hayo hadi soko la Nyashimbi lakini kwa sasa hatupo eneo hilo na sasa hakuna mkandarasi anayesomba uchafu katika eneo hilo,” amesema Afisa huyo.