Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imekabidhi jumla ya meza 18 na viti 18 kwa Shule ya Sekondari Mazinge iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuunga mkono jitihada za kuinua elimu.
Akikabidhi msaada huo, Meneja Msaidizi wa Huduma kwa Mlipakodi wa TRA Shinyanga, Ramadhani Sengo, amesema lengo ni kuwahamasisha wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao ili kufanikisha ndoto zao na hatimaye kuwa miongoni mwa watoa huduma muhimu kwa taifa, ikiwemo ukusanyaji wa kodi.
“Madawati haya ni hamasa kwa watoto wetu kusoma kwa bidii zaidi. Huenda siku moja wakawa miongoni mwa wakusanya kodi wa taifa letu. Tunaomba vitunzwe na kutumika kwa manufaa ya wote,” amesema Sengo.
Viongozi wa shule hiyo wameishukuru TRA kwa msaada huo na kueleza kuwa utapunguza changamoto ya upungufu wa samani na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.