
HISPANIA: Takribani watu 30 wamefariki dunia na wengine 80 kujeruhiwa baada ya treni mbili za mwendo kasi kugongana katika eneo la mkoa wa Toledo, katikati mwa Hispania, Jumatano asubuhi, Oktoba 28, 2026.
Taarifa za mamlaka za eneo hilo, ajali hiyo imetokea kati ya miji ya Mora, Orgaz na Urda, katika mkoa wa Toledo, huku shughuli za uokoaji zikiendelea katika eneo la tukio.
Msemaji wa serikali ya eneo la Castilla-La Mancha, Esther Padilla, alithibitisha kuongezeka kwa idadi ya waliofariki kutoka watu 10 waliokuwa wametangazwa awali, akionya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka zaidi kadiri shughuli za uokoaji zinavyoendelea.
Rais wa eneo hilo, Emiliano García-Page, alisema watu 80 wamejeruhiwa, ambapo 50 kati yao wamepata majeraha ya wastani hadi makubwa.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa treni hizo mbili zilikuwa zikisafiri kutoka Madrid kuelekea Seville wakati ajali ilipotokea.
Treni moja inayomilikiwa na kampuni ya serikali ya Renfe ilikuwa na abiria 397, huku treni nyingine inayomilikiwa na kampuni binafsi ya Iryo ikiwa na abiria 147.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, treni moja iligonga nyingine iliyokuwa imesimama, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mabehewa kadhaa yaliyotoka kwenye reli.
Picha kutoka eneo la tukio zimeonesha mabehewa yaliyoharibika vibaya, huku vikosi vya uokoaji vikifanya kazi ya kuwatafuta na kuwasaidia manusura.
Hata hivyo, chanzo kamili cha ajali hiyo hakijawekwa wazi katika taarifa za awali.
WAZIRI MKUU WA HISPANIA ATOA SALAMU ZA POLE
Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ameeleza kushtushwa na ajali hiyo na kutoa pole kwa waathirika pamoja na familia zilizopoteza ndugu zao.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Sánchez alisema huduma za dharura zinaendelea kutoa msaada kwa walioathirika na kuhakikisha usalama wao, kwa kushirikiana na mamlaka zote zinazohusika.
Alieleza mshikamano wake kwa waathirika na familia zao katika kipindi hicho kigumu.
SHUGHULI ZA UOKOAJI ZAENDELEA
Ajali hiyo imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa usafiri wa reli nchini Hispania, huku mamlaka zikiendelea kushughulikia madhara ya tukio hilo na kukusanya taarifa zaidi.
Kwa sasa, juhudi zinaendelea kuwasaidia majeruhi na kubaini mazingira yaliyosababisha treni hizo kugongana.
Taarifa zaidi kuhusu uchunguzi wa ajali hiyo, utambulisho wa waathirika na hatua zitakazochukuliwa na mamlaka zinatarajiwa kutolewa kadiri taarifa rasmi zitakavyopatikana.
