Vijana 147 kati ya 67,299 waliojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria katika kipindi cha miaka mitatu wamekutwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Takwimu hizo ni sawa na asilimia 0.22 kwa vijana waliomaliza kidato cha sita nchini na ambao waliitwa kujiunga na JKT katika kipindi cha miaka hiyo 2019, 2020 na 2021.
Hayo yamo katika taarifa ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kwa kipindi cha Februari 2022 hadi Februari 2023 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma jana Ijumaa, Februari 3, 2023.
Taarifa hiyo, iliwasilishwa na Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Massare akieleza hali bado si nzuri katika maambukizi mapya ya VVU ingawa kitakwimu kumekuwa na upungufu kwa kila mwaka.
Kamati hiyo imependekeza mkakati wa kupima na kuzuia maambukizi mapya ya VVU uongezwe. Pia pawepo na juhudi za makusudi katika lishe kwa wafungwa wenye maambukizi hasa Gereza la Isanga jijini Dodoma.
Kwenye taarifa hiyo, inaonyesha mwaka 2019, vijana waliojiunga JKT walikuwa 20,413 huku 60 wakikutwa na maambukizi wakati 2020 walijiunga vijana 21,383 na maambukizi yalikuwa kwa vijana 45 na mwaka 2021 walijiunga vijana 25,503 na 42 kati yao ndiyo walikutwa na VVU.
“Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu, yaani 2018 hadi 2021, Jeshi la Kujenga Taifa limechukua vijana kwa mujibu wa sheria ambapo vijana wenye Virusi vya Ukimwi katika Jeshi la Kujenga Taifa wanapatiwa huduma mbalimbali kama vile ushauri nasaha kabla ya kupimwa VVU,” alisema Masale.
Mbunge huyo alisema, hakuna sheria au utaratibu wa kuwarudisha majumbani vijana wanaobainika kuwa na maambukizi kama ilivyo kwa wanaokutwa na mimba ambao ndiyo hurudishwa majumbani.