Kwa mara nyingine mwigizaji na mtayarishaji wa filamu nchini, Idris Sultan ameingia kwenye soko la filamu la kimataifa baada ya filamu aliyoshiriki ya Married to Work kuingia kwenye mtandao wa kusambazaji na kuonyeshaji wa filamu wa Netflix.
Filamu hiyo inayotarajiwa kutoka Februari 10 mwaka huu kupitia mtandao wa Netflix imeigizwa kwenye nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Nigeria, huku ikiwahusisha waigizaji wakubwa kutoka nchi hizo.
Hii ni mara ya pili kwa Idris kuonekana kwenye mtandao huo wa kimataifa baada ya mara ya kwanza kuonekana kupitia filamu ya Slay iliyotoka mwaka 2021.
Akizungumza Februari 5, 2023 Idris amesema soko la filamu za kiswahili linakua kwa kasi kutokana na juhudi zinazofanywa na wasanii pamoja na watayarishaji wazawa.
Amepongeza jitihada za kila mmoja aliyefanikisha uwepo wa filamu ya Married To Work kwenye mtandao huo wa usambazaji filamu duniani.
“Ubunifu wetu kwenye sanaa unakua siku hadi siku, kama Taifa hatua hii inatufungulia masoko ya kimataifa na majukwaa makubwa ya filamu, tunafanya watu watufuatilie” amesema Idris.
Idris pia ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya soko la filamu kupitia filamu ya ‘Royal Tour’ ambayo imeitambulisha nchi katika soko la kimataifa.
Aidha ameongeza kwa kuwataka mashabiki na wapenzi wa filamu, wasikose kufatilia mtandao huo wa Netflix ifikapo February 10, kwa ajili ya kuangalia filamu hiyo ili kuzidi kuwapa tumaini ili wawekeze zaidi Tanzania.
Mbali na uigizaji, upigaji picha Idris alikua Mtanzania wa pili kushinda shindano la Big Brother Hotshots mwaka 2014 na kuzawadiwa Dola za Marekani 300,000 sawa na Sh500 milioni, baada ya Richard Dyle Bezuidenhout kuibuka shujaa mwaka 2011 katika Big Brother II.