Wakati Yanga ikijiandaa na safari ya kuwafuata US Monastir katika mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika, kuna nafasi kubwa winga wake, Bernard Morrison kukosa msafara huo.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa hadi sasa wakibakiza saa 48 kabla ya kuanza safari ya kwenda Tunisia ni Morrison pekee ambaye anaweza kukosa mchezo huo.
Nabi alisema Morrison raia wa Ghana aliumia nyonga akiwa kwao na kwamba anaweza kukaa muda mrefu zaidi kutokana na tatizo hilo.
“Aliporudi hapa alikuwa tayari na maumivu, nadhani huyo ndiye mchezaji anayetupa wasiwasi wa kumkosa, yupo katika matibabu ya majeraha hayo,” alisema Nabi.
Hata hivyo, Nabi alisema bado wana kikosi kipana ambacho kitawapa nafasi ya kupata winga mwingine, ingawa alikiri mawinga wake wengi bado hawajamkosha msimu huu.
“Tuna watu wa kuchagua kuweza kuziba nafasi yake, hii ni timu ambayo tunafanikiwa kutokana na kuweka ubora sawa kutoka mchezaji mmoja kwenda mwingine.
“Tuna idadi nzuri ya mawinga, lakini changamoto kubwa tuliyonayo wengi wao bado hawajacheza kwa ubora tunaoutaka, kumekuwa na panda kushuka nyingi katika ubora wao,” aliongeza Nabi.
Msimu huu, Morrison amefanikiwa kuichezea Yanga katika michezo 10 pekee, mara ya mwisho kuichezea Yanga ilikuwa Desemba 25, wakati vinara hao wa Ligi Kuu wakishinda dhidi ya Azam. Ameshakosa mechi tatu za ligi pekee.
Yanga itaondoka Jumatano, kuifuata US Monastir nchini Tunisia, mchezo utakaofanyika Februari 12, kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet, jijini Tunis.
Kiwango cha ligi
Kocha wa miamba hiyo, Nabi alisema anaamini mchezo utakuwa mzuri kutokana bna jinsi kikosi chake kinavyoendelea kujiandaa kikitoka kupata ushindi dhidi ya Namungo FC.
Nabi alisema Namungo ni moja ya timu ngumu za Ligi Kuu Tanzania Bara, na kuwa kipimo kizuri kabla ya mchezo wa kimataifa dhidi ya US Monastir.
“Matarajio ni kufanya vizuri, tulikuwa na mchezo bora dhidi ya Namungo, japo tulipoteza umakini kwa baadhi ya matukio, lakini kimekuwa kipimo kizuri,” alisema.