Takriban nyumba 46,000 zimekatikiwa umeme wakati kimbunga Gabrielle kikishambulia kaskazini mwa New Zealand. Mamlaka zimetoa tahadhari juu ya mvua kubwa na upepo, na mamia ya safari za ndege zimefutwa.
Baadhi ya maeneo yametangaza hali ya hatari, wakati kimbunga Gabrielle ikikaribia kisiwa cha Kaskazini. Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya mji wa Auckland na maeneo jirani kukumbwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na kusababisha vifo vya watu wanne.
Waziri wa usimamizi wa dharura Kieran McAnulty aliambia mkutano wa vyombo vya habari siku ya leo kwamba serikali inafikiria kutangaza hali ya hatari ya kitaifa kwa mara ya tatu tu katika historia ya nchi hiyo.
Hali ya hatari tayari imetangazwa katika mikoa mitano ya kaskazini ikiwemo Auckland. Tamko hilo linazipa mamlaka zaidi mamlaka ya serikali za mitaa kukabiliana na hali hatarishi na kuziruhusu kuzuia usafiri na kutoa misaada.