Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema kuwa, wanalazimika kumlipa mshahara mkubwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mghana, Bernard Morrisson kutokana na uzoefu na mchango wake mkubwa katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mghana huyo yupo nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza maumivu ya nyonga.
Morrison aliyesajiliwa kwa dau la zaidi ya Sh 300Mil, huku akilipwa mshahara wa 20Mil, ameikosa michezo miwili ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia na TP Mazembe ya DR Congo.
Kwa mujibu wa Hersi, kiungo huyo ni kati ya wachezaji wanaolipwa fedha nyingi kutokana na ubora, uzoefu alionao wa kucheza michuano ya kimataifa ambayo malengo yao siku moja kuja kubeba taji hilo.
“Morrison analipwa fedha nyingi kwa kiwango kikubwa, hiyo ni kutokana na uzoefu wake mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa ambayo tunashiriki, hivyo anaweza kuwa na mchango mkubwa sana.
“Yanga tumemrudisha kikosini, lakini bado hajaonesha kile ambacho wengi walikitarajia, hapo sasa ndio suala la mkataba linapokuja.
“Mchezaji ana mkataba na anatakiwa kuuheshimu, atalipwa awe anacheza au hachezi. Mchezaji ameumia lakini wakati anasajiliwa alikuwa mzima, aliumia wakati akiitumikia Yanga. Mchezaji akiumia hawezi kucheza. Hiyo haiepukiki
“Hivyo kama uongozi tunamuhudumia na huu ndio uungwana ambao Yanga unao. Tunamuhudumia kuhakikisha anakuwa bora kuelekea mwishoni mwa msimu au baadae,” alisema Hersi