Manchester United wamefikia makubaliano na Alejandro Garnacho juu ya kuongeza mkataba wa miaka mitano, hii ni kwa mujibu wa ripoti za michezo huko England.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18, mkataba wake wa sasa unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu ujao na klabu kama Real Madrid na Juventus zimeonyesha nia ya kutaka saini yake.
Hata hivyo, Garnacho ameonekana kufurahia maisha ya Old Trafford ndio maana anataka kuendelea kubaki kwenye viunga vya Manchester.
ESPN inaripoti kwamba winga huyo amekubali mkataba wa miaka mitano United ambao utakuwa na nyongeza kubwa ya mshahara na bonasi mbalimbali.
Muargentina huyo ameendelea kuonesha kiwango kizuri, na msimu huu hadi sasa amefunga mabao matatu na kutengeneza asisti tano katika michuano yote.