Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Makeremo Luhanga, Mkazi wa Kitongoji cha Kitete, wilayani Chunya kwa mahojiano kutokana na vifo vya watoto wake wawili baada ya kunywa vitu vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kienyeji
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Benjamani Kuzaga amethibitisha kukamatwa kwa Luhanga Februari 19 majira ya saa mbili asubuhi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu vifo vya watoto baada ya kunywa dawa ya kienyeji kutoka kwa mganga aliyefahamika kwa jina moja la Galwinzi wa Kijiji cha Goririma wa eneo la Lupa.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina kutokana na watoto wa familia ya mzee Makeremo kusumbuliwa na maradhi ya tumbo na vichomi kwa muda mrefu hivyo kuamini matatizo hayo yanatokana na kulogwa,” amesema Kamanda Kuzaga.
Amewataja watoto waliofariki dunia kuwa ni Mafunda Makaremo(18) na Raphael Makaremo (26) huku wengine watatu ambao ni Nchambi Lusangija (50), Manyilizu Kulyehlwa (07) na Njile Makeremo (18) wakiendelea kupata matibabu Hospitali ya Wilaya ya Chunya baada ya kunywa dawa hizo za kienyeji na hali zao zinaendelea kuimarika.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina kutokana na watoto wa familia ya mzee Makeremo kusumbuliwa na maradhi ya tumbo na vichomi kwa muda mrefu hivyo kuamini matatizo hayo yanatokana na kulogwa,” amesema Kamanda Kuzaga.
Ameongeza kuwa msako unaendelea kumtafuta mganga wa kienyeji ambaye alikimbia baada ya tukio hilo na kutoa wito kwa jamii kuachana na imani potofu za kishirikina kwani zina sababisha madhara makubwa kwa jamii na badala yake watafute tiba ya maradhi yanayowasumbua kwa kwenda Hospitali kwa ajili ya vipimo na matibabu kutoka kwa matabibu.
Aidha amewataka kuacha tabia ya kuwatumia waganga wa kienyeji wasio na vibali ambao wana walaghai kuwatibu kwa kutumia dawa za kienyeji kwa lengo la kujipatia kipato pasipo kuwa na uelewa wa dawa wanazozitoa bila vibali.