Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka 40 ambao unawahusisha wakulima na wafugaji katika vitalu vinne vilivyoko katika kijiji cha Kashanda kata Nyakahanga wilayani Karagwe, hatimaye umetatuliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Julius Laizer kwa kugawa vitalu viwili kwa wakulima na viwili kwa wafugaji.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, baadhi ya wananchi na viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, wamesema kuwa kuwepo wa mgogoro huo kwa muda mrefu, kumesababisha kushindwa kutumia ardhi yao kuongeza kipato, huku wakishukuru kwa hatua hiyo.
“Mungu ameona, alichokiona juu ya wakulima wa Kijiji Kashanda ni kuwatuma watu ambao wana moyo wa kutusaidia” wamesema wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Julius Laizer amewataka wakulima na wafugaji waliovamia maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli zao kuondoka mara moja.
“Wakulima mnajua mlikokuwa mnalima, mnajua wakulima wapya na walikotoka wakaja kuanzisha mashamba mapya, orodha ninayo, kama mmefyeka misitu na kulima kwenye vyanzo vya maji ondoka kwa ustaarabu wako, wapo wafugaji hapa wamepewa vitalu na halmashauri hawalipi kodi, umeona kitalu chetu hakikustahili ondoka” amesema Laizer.