Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Erasmus Swai amembwaga kortini Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) aliyekata rufaa dhidi yake kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai kumwachia huru katika kesi ya ubakaji.
Januari 1, 2021 padri huyo alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, akishtakiwa kwa makosa ya kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha nne, mwenye umri wa miaka 16.
Mara baada ya kufikishwa mahakamani, uongozi wa kanisa hilo Jimbo la Moshi ulimwandikia barua ya kumsimamisha padri huyo kutoa huduma, wakati huo akihudumu katika Parokia ya Manushi Sinde, hadi uamuzi wa mahakama utakapotolewa.
Upande wa mashtaka ulikuwa unadai kuwa padri huyo alitenda makosa hayo Machi mwaka 2020 katika Hoteli ya Snow View iliyopo Mji mdogo wa Bomang’ombe wilayani Hai, makosa ambayo hata hivyo mshtakiwa liyakanusha.
Machi 3, 2021, Mahakama hiyo ikakubali ombi la upande wa mashtaka la kufanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kama mtoto aliyezaliwa alikuwa ni mtoto wa padri huyo, hata hivyo majibu yake hayakuwahi kuwekwa wazi.
Wakati kesi ikiendelea, Agosti 17, 2021, upande wa mashtaka uliomba kubadili hati ya mashtaka na kuondoa shtaka la kumpa mimba mwanafunzi huyo na kubakiza shtaka moja la kubaka.
Baadaye mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi, Thurstone Kombe iliifuta kesi hiyo Oktoba 21, 2021 baada kuahirishwa zaidi ya mara nane huku kila wakati upande wa mashtaka ukitoa sababu mbalimbali za kuomba kesi iahirishwe.
Mahakama ilikuwa imetoa ‘ahirisho la mwisho’ mara nne lakini amri zote hizo za mahakama hazikuheshimiwa na siku hiyo upande wa mashtaka ukaomba kesi iahirishwe tena kwa sababu mwendesha mashtaka hakuwa na jalada la polisi la shauri hilo, ndipo hakimu akaifuta.
DPP hakuridhika na uamuzi huo akakata rufaa k akieleza kuwa hakimu alikosea kumfutia mashtaka padri huyo na kumwachia huru bila kutaja kifungu cha sheria kinachompa mamlaka hayo.
Katika rufaa hiyo, padri huyo alitetewa na wakili Hellen Mahuna wakati DPP aliwakilishwa na wakili wa Serikali Marry Lucas.
Uamuzi wa Jaji
Katika hukumu yake iliyowekwa katika mtandao wa Mahakama Kuu jana, Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi aliitupilia mbali rufaa akisema mahakama ua Hai iliuvumilia sana upande wa mashtaka na mshtakiwa aliachiwa kwa usahihi.
“Nimeridhika upande wa mashtaka ulivuruga utoaji wa haki kwa mahakama, naomba kusisitiza maoni yangu kwa kanuni inayokubalika ya haki inayosema si tu haki itendeke, bali pia ionekane inatendeka,” alieleza Jaji Kilimi.
“Kwa maoni yangu kwa kuzingatia kanuni hiyo na mazingira ya usikilizwaji wa kesi hii sina shaka hata kidogo upande wa mashtaka ulitumia vibaya utaratibu wa kisheria na haupaswi kuachwa bila kuguswa,” alisisitiza Jaji huyo.
Jaji Kilimi alisema anafahamu kwa mamlaka aliyonayo DPP anapaswa kuheshimu misingi ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya mchakato wa kisheria, masilahi ya umma na kudhibiti mwenendo wa mashauri ya jinai”
Alifafanua kuwa kwa msingi huo, DPP alikuwa na nafasi ya kuiondoa kesi hiyo kwa njia ya nolle prosequi (kutokuwa na nia ya kuendelea nayo) kama iliamini hana ushahidi wa kuendesha kesi hiyo katika kipindi chote hicho na mahakama ingetimiza wajibu wake wa kumwachia mtuhumiwa.
“Kuondoa kesi mahakamani kwa utaratibu huo haumzuii kumkamata tena na kumshtaki mtuhumiwa kwa mashtaka yaleyale lakini hili halikufanywa na upande wa mashtaka na kwa kile walichokifanya wao ndio walikuwa wanaishawishi mahakama iiondoe,” alisema.
Jaji alikataa kuirudisha kesi hiyo mahakama ya wilaya ya Hai ili itoe amri ya kumwachia na si kufuta mashtaka kwani kwa kufanya hivyo, upande wa mashtaka utamkamata tena na itakuwa si kumtendea haki mshtakiwa. “Kwa maoni yangu … hii itamtia hatarini mtuhumiwa kinyume na kanuni ya usawa mbele ya sheria”.