China imemhukumu raia wa Marekani kifungo cha maisha jela kwa kosa la ujasusi, mahakama ilisema jana na kufichua maelezo machache kuhusu kesi hiyo ambayo haikuripotiwa awali.
John Shing-wan Leung (78) mwenye makazi ya kudumu Hong Kong, alipatikana na hatia na kufungwa maisha jela, kunyimwa haki za kisiasa, ilisema taarifa kutoka kwa mahakama moja katika mji wa Suzhou mashariki mwa China.
Mamlaka ya Suzhou ilichukua hatua za lazima kulingana na sheria dhidi ya Leung Aprili 2021, ilisema bila kutaja ni lini aliwekwa kizuizini. Msemaji wa Ubalozi wa Marekani mjini Beijing alisema wanafahamu taarifa kwamba raia mmoja wa Marekani alipatikana na hatia hivi karibuni na kuhukumiwa.
“Wizara ya Mambo ya Nje inazingatia zaidi kipaumbele cha usalama wa raia wa Marekani waishio nje ya nchi,” alisema msemaji huyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Wang Wenbin alikataa kutoa maoni zaidi juu ya kesi hiyo katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari.
Huko Hong Kong, Waziri wa Usalama, Chris Tang aliambia mkutano wa wanahabari jana mamlaka ya jiji hilo iliarifiwa kuhusu kukamatwa kwa Leung mwaka 2021.
“Polisi wa Hong Kong wamefanya ufuatiliaji kulingana na taarifa,” Tang alisema, akikataa kufafanua zaidi. Kufungwa huko kuna uwezekano wa kuharibu zaidi uhusiano na Marekani ambao tayari umezorota katika masuala kama vile biashara na haki za binadamu.
Marekani na China zimemaliza muda usio rasmi wa kusitisha mawasiliano ya ngazi ya juu kuhusu hatua ya Marekani ya kuitungua Februari puto inayoshukiwa kuwa ya uchunguzi wa kichina.
Mshauri wa Usalama wa kitaifa wa Marekani, Jake Sullivan na mwanadiplomasia mkuu wa China, Wang Yi walifanya mazungumzo mjini Vienna katika mafanikio yaliyoonekana wiki iliyopita na pande zote mbili zikiuelezea mkutano huo kuwa “wazi, muhimu na wenye kujenga”.