Watu wenye silaha Jumanne walishambulia msafara wa wa magari ya Marekani katika jimbo la kusini mashariki mwa Nigeria la Anambra, polisi na afisa wa Marekani wamesema. Washambuliaji hao waliwaua watu wanne na kuwateka nyara wengine watatu.
Watu wanaotaka kujitenga ambao wanaendesha harakati zao katika eneo hilo walizidisha mashambulizi yao katika miaka ya hivi karibuni, wakilenga hasa polisi na majengo ya serikali.
“Hakuna raia wa Marekani aliyekuwa katika msafara huo,” msemaji wa polisi Ikenga Tochukwu alisema.
Watu hao wenye silaha “waliwaua maafisa wawili wa jeshi la polisi na wafanyakazi wawili wa ubalozi mdogo wa Marekani,” kabla ya kuchoma moto gari lao,” msemaji huyo wa polisi ameongeza.
Shambulio hilo lilifanyika Jumanne saa tisa na nusu alasiri majira ya huko kwenye barabara ya Atani, Osamale katika wilaya ya Ogbaru, kulingana na polisi.
Kikosi cha pomoja cha polisi na jeshi kilipelekwa kwenye eneo la tukio, alisema Tochukwu, lakini watu hao wenye silaha waliweza kuwateka nyara maafisa wawili wa polisi na dereva.
Msemaji wa Baraza la usalama wa taifa wa Marekani John Kirby alithibitisha shambulio hilo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Washington.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilithibitisha pia shambulio hilo.