Ni rasmi sasa ombi la wafanyabiashara wote wa Kariakoo kushiriki mkutano na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa limekubaliwa ambapo sasa utafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Wafanyabiashara hao ambao awali walipaswa kutoa wawakilishi wao kwenye kikao na Waziri Mkuu walikataa pendekezo hilo huku wakishinikiza uwepo wao wote ili kuleta tija ya maamuzi ya mkutano huo.
Mmoja wa viongozi wa wafanyabiashara hao (jina lake halikupatikana kwa haraka) ambaye alifanya kikao cha ndani na baadhi ya viongozi wa Serikali alitoka nje na kutoa tamko kuwa wafanyabiashara wote watashiriki mkutano na Waziri Mkuu.
“Wote tutashiriki mkutano na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) katika viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo tutaenda hata kwa miguu,”amesema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Kauli hiyo iliibua shangwe kwa wafanyabiashara waliofurika nje ya ukumbi wa Arnaoutoglou wakiimba wimbo wa kuwa na imani na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ni saa tano sasa zimepita tangu wafanyabiashara hao kukita kambi nje ya ukumbi huo wakimsubiri Waziri Mkuu Majaliwa kwa ajili ya mkutano huo.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wameendelea na mgomo wa kufungua maduka yao siku ya tatu kwa ajili ya kushinikiza kutolewa kwa kodi ya stoo na kukomeshwa kwa kile wanachokiita kamatakamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).