Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema majukumu aliyopewa na Rais samia Suluhu Hassan, yamemfanya akue mara mbili zaidi.
Mkuu huyo wa mkoa amemuahidi Rais kuwa, ategemee mambo makubwa kutoka kwake, watendaji waliochini yake na kwa ushirikiano mkubwa toka kwa wakuu wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Chalamila ameyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa minara ya kurusha matangazo ya Azam Media inayofanyika jijini hapa.
“Wakati naapishwa kwenda Kagera uniambia unaamini akili yangu imetulia, nataka nikuhakikishie kuwa majukumu uliyonipa yamenifanya nikuwe mara mbili. Nakuahidi utegemee mambo makubwa kutoka kwangu na kwa ushirikiano mkubwa na wakuu wangu wa wilaya zote,” Amesema Chalamila na kuongeza.
“Wakurugenzi, Makatibu tawala, wote hawa nakuahidi kuwa tutashirikiana kwa kiasi cha kutosha kusogeza maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam.”
Aidha ‘bosi’ huyo wa Dar es Salaam amesema kuwa mkoa uko katika mikono salama na kwamba atahakikisha ofisi za umma hazina watu wala rushwa, wanaopenda majungu, wasiokuwa na ushirikiano na wasiolinda sifa yake, hali ya unyang’anyi na dhuruma itakomeshwa na kusikiliza zaidi Watanzania.
“Naomba uendelee kuniamini na ninaamini utaendelea kuniamini pia,” alisema Chalamila.
Amesema jana alianza kazi rasmi kwa kushirikiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutatua matatizo ya wafanyabiashara ambayo ilikuwa ni utekelezaji wa maagizo yake.
“Kwa hakika aliweza kumaliza mgogoro ule, nikuthibitishie kuwa kwa kadri nilivyokaa na viongozi wenzangu, hii tabia ya migogoro mpaka inafika katika ngazi yako, haitajirudia tena,”
Amesema wamejipanga kuhakikisha kuwa matatizo yote yanamalizwa kabla ya kufika katika ngazi ya Rais.