Baada ya miezi kadhaa ya matarajio, Gavana wa Florida nchini Marekani Ron DeSantis aliingia rasmi katika kinyang’anyiro cha mchujo wa urais wa chama cha Republican siku ya Jumatano, akinuia kugombea urais mwakani.
Kufikia sasa, anachukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa rais wa zamani Donald Trump katika uwanja wa siasa wenye wawaniaji wengi, kwelekea kwa uchaguzi wa mwakani, lakini wapiga kura wengi wanaanza tu kumjua gavana huyo mwenye umri wa miaka 44.
Haya hapa ni mambo matano ya kujua kuhusu DeSantis, muwaniaji mpya zaidi wa uteuzi ili kugombea urais kwa tikiti ya chama cha Republican:
Maisha ya mapema ya Desantis
Mzaliwa wa Florida aliye na asili ya kifamilia huko Midwest, DeSantis alikuwa mchezaji bora wa mpira wa baseball katika miaka yake ya ujana. Aliwakilisha timu ya Dunedin, Florida, kwenye Msururu wa Ligi Ndogo ya Dunia ya 1991 kabla ya kuwa kapteni wa timu ya Chuo Kikuu cha Yale.
Baada ya muda mfupi wa kufundisha shule ya upili, aliendelea kusomea sheria katika chuo kikuu cha Harvard. Kisha akawa mwanasheria wa Jeshi la Wanamaji, nafasi ambayo ilimpeleka Iraq na kambi ya kizuizini ya Guantanamo Bay.
DeSantis aligombea ubunge mnamo mnamo 2012, na kushinda uchaguzi na kuwa mwakilishi wa wilaya ya Orlando na kuwa mwanachama mwanzilishi wa vuguvugu la kisiasa la mrengo wa kulia kwenye baraza la wawakilishi.
Kama wahafidhina wengi katika bunge wakati huo, alitetea mabadiliko ya mfumo wa afya na Usalama wa Jamii, ikiwa ni pamoja na hatua moja ambayo ingeongeza umri wa kustaafu hadi 70.
Mgombea atakayeteuliwa atachuana na Rais Joe Biden , mdemocrat katika uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka kesho.