Kama ulifikiri mabadiliko ya teknolojia na jamii kuchangamana kumeua mila na desturi kwa Watanzania wengi, umekosea. Kama unadhani watu wakisoma na kupata madaraka wanasahau asili zao umepotea, Bernard Kamilius Membe alikuwa miongoni mwa waliokataa utumwa wa kusahau asili yao.
Huyu alikuwa mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliyefariki dunia Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki, Dar es Salaam na kuzikwa kijijini kwake Rondo, Kata ya Chiponda, Mei 16, 2023.
Nyumba ya Membe ipo ndani ya uzio wa ukuta katika eneo la ardhi lisilopungua ekari mbili, ndani yake kuna mandhari ya kuvutia inayotokana na bustani ya maua, miti ya aina mbalimbali, ukiwemo ‘msufi pori’ ambao umebatizwa mti wa maajabu na wengine huuita wa ‘maamuzi magumu’.
Umaarufu wa mti huu na sifa zake huwezi kuusikia nje ya nyumba ya Membe au mbali na Rondo, umebeba historia lukuki ya kimila, kisiasa na kijamii.
Licha ya nyumba hiyo kuwa na miti mingi mikubwa inayotoa kivuli iliyopo katika bustani nzuri inayohudumiwa kwa viwango vinavyotakiwa, msufi pori umeendelea kuwa ndani ya mioyo na machoni mwa wakazi wa Rondo.
Chini ya mti huu, Membe na wanakijiji wenzake walikuwa wakikutana na kuzungumzia masuala yanayohusu jamii yao au Taifa.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anaweza kuwa mmoja wa kuuelezea vizuri mti huu, kwa kuwa hata kikao cha kutambulishwa kwa wazee kuwa ndiye atakayerithi mikoba ya ubunge aliokuwa akiushikilia Membe katika jimbo la Mtama mwaka 2015 vilifanyika chini ya mti huu.
Najua hataweza kusahau namna wazee wa Rondo walivyomkatalia Membe kuwa hawaoni mtu mwingine atakayeweza kuvaa viattu vyake (ubunge) licha ya Membe kuwasisitiza Nape ni mtu sahihi kwa jimbo la Mtama. Kilichofuatia ni historia hivi sasa.
Chini ya mti huu, Membe alikabiliana na wakati mgumu wa kuwaelimisha ‘wazee’ kwa nini atakwenda kuwania urais na anaacha ubunge aliodumu nao kwa takriban miaka 10.
Kama mti huu ungekuwa unazungumza, si ajabu tungeyajua mengi ya siri na wazi yaliyosemwa na kufanywa ukishuhudia.
Mti wa maamuzi magumu, sasa umempoteza Chifu wa Rondo ambaye kila sherehe za mwisho wa mwaka hakukosa kuwaalika wanajamii kwa ajili ya kumwagilia moyo kwa kinywaji, vyakula na posho ya kustaftahi siku ya inayofuata.
Chini ya mti huu ‘wazee’ walikuwa wakipata tabu kumuelewa Membe juu ya kauli na uamuzi aliokuwa akifanya, lakini walikubaliana na misimamo yake ya kupenda haki, utu, heshima, demokrasia na uhuru.
Wakati wa utawala wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, mti huu ulipata shida zaidi maana kulikuwa na vikao vingi kumsihi Membe asichukue hatua au kutoa kauli zilizokuwa hazifurahishi watawala.
Mara kadhaa Membe amepata kuelezea kuwa mti huo wenye zaidi ya miaka 30 kama wangeamua kuukata na kupasua mbao wangetoa zaidi ya 300, lakini hawajafanya hivyo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo za kimila, kivuli na makutano ya wanajamii.
Chini ya mti huu Membe ndipo alipotangaza kutokuwa tayari kunyamazia ukiukaji wa haki za bindamu, kuminya demokrasia na kutofuata utawala wa sheria kulikokuwa kukifanywa wakati wa utawala wa awamu ya tano.
Ni wakati huo alipowaambia wazee, vijana na wanawake kuwa yupo tayari kubakia peke yake kuliko kuendelea kunyamazia mambo yaliyokuwa hayaendi sahihi kisa yalikuwa yakifanywa na mtu au watu wenye madaraka.
Chini ya mti huu, Membe aliieleza jamii yake dhamira ya kujiunga na ACT-Wazalendo kuendeleza demokrasia baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumfukuza uanachama kutokana na mienendo isiyofaa.
Hakueleweka na aliwapa wakati mgumu wenzake kushirikiana naye akiwa upande wa pili kwa kuwa wengi walikuwa CCM.
Mti huu ungeweza kusema baadhi ya jamii yake walivyokuwa wakienda nyumbani kwake kwa kificho kukwepa kushughulikiwa na utawala ambao ulishamuona Membe ni tatizo.
Mti huu unaweza kusema mafuriko ya watu yalivyorejea nyumbani hapo Mei 29, 2022 baada ya Membe kurejea CCM na kutangaza hatohama tena CCM hadi anaingia kaburini kwa kuwa sababu zilizomuondoa ndani ya chama hicho hazikuwapo tena.
Ni kweli mpaka anaingia kaburini Membe hakuondoka CCM, mwili wake ulishushwa kutoka ndani ya gari, helikopta na kuingizwa kaburini na vijana kutoka Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Membe ameondoka na siri nyingi moyoni mwake, msufi pori umebaki na siri nyingi na hauna uwezo wa kuzisema.
Mzee wa kimila
Akizungumza na Mwananchi wakati wa msiba wa Membe, Mzee wa kimila kutoka kabila la Wamwera, Amour Mkombelo alisema siri ya mti huo una maajabu kwa kuwa magamba yake yakichemshwa na maji yake akioga mtu nuksi zinamuondokea na mambo yanamnyookea.
“Huu mti aliupanda Membe miaka 50 au 60 iliyopita akiwa kijana, tunapokaa katika mti huu na kujadili mambo yetu hata yawe magumu vipi yanakuwa mepesi, hata kama hatuna mawazo mazuri tunayapata ndiyo maana tunauita mti wa maajabu,” anasema.
Mkombelo alisema nyakati za uchaguzi wanapokaa kwenye mti huo kujadili kiongozi wanayemtaka matokeo yake huwa mazuri zaidi, hivyo mti huo unaendelea kuaminika.
Anasema pia shughuli za kimila hufanyika katika mti huo kwa nyakati mbalimbali kulingana na mazingira.
“Si Wamwera pekee wanaojua faida za mti huu, bali hata makabila mengine yamekuwa yakifika hapa na kuendesha shughuli za kimila ambapo matokeo yake huwa mazuri, tulibahatika mti huu kuwa nyumbani kwa Membe ambaye naye alikuwa mtu wa watu na kiongozi wetu wa kisiasa na kimila, kifo chake ni pigo kubwa kwetu,” alisema.
Mkombelo anasema mti huo si wa maajabu kwa Membe pekee na hautaishia kwa mwanasiasa huyo, bali unahusisha jamii yote, hivyo wataendelea kuutunza na wanaamini familia haitazuia watu kuutumia.
Rukia Said alisema anaamini Rondo ilibarikiwa kupata mti huo uliokuwapo nyumbani kwa mwanasiasa aliyejitolea kusaidia jamii bila kujali wadhifa na elimu aliyokuwa nayo.
“Kuna nyakati tulikuwa tukikaa vikao vya kujadiliana namna ya kwenda kuomba msaada kwa wahisani kwa ajili ya maendeleo yetu tukiwa chini ya mti huu na tukienda kuomba hatuchukui muda mrefu.
chini ya yenye kutoa kivuli Chini ya, ajani iyopambwa
Safari inaanza kutoka Dar es Salaam, jiji lenye kila tafsiri ya Utanzania. Unafuata uelekeo wa Mbagala unaivuka hadi Kongowe. Miji inabadilika kutoka Kimanzichana hadi Kibiti. Ramani ya Google inautafsiri mwendo kuwa tunakatiza kando ya Bahari ya Hindi.
Vipimo vinaonesha kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Lindi ni umbali wa kilometa 460 kama unasafiri kwa gari, na kilometa 356 ikiwa unapaa kwa ndege. Ni safari ya hisia. Kwenda kumpumzisha mmoja wa watoto halisi wa Tanzania, aliyeyatoa maisha yake kuutumikia umma.
Bernard Kamillius Membe, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70 kasoro miezi sita. Miaka zaidi ya 40 aliyoutumikia umma wa Watanzania kabla ya kustaafu, kikokotoo chake kinaonesha kuwa takriban asilimia 64 ya maisha aliyatumia kuihudumia Jamhuri.
Bahati mbaya, hakuna tathmini ambayo inaweza kutoka ili kujenga makisio japo ya kifikra ni kiasi gani Tanzania leo ina unafuu mkubwa kwa sababu ya utumishi uliotukuka wa Membe.
Shairi la “Character of the Happy Warrior” – “Uhusika wa Shujaa Mwenye Furaha”, lililoandikwa na mwandishi wa UK, William Wordsworth, Septemba 3, 1802, linaweza kutusaidia kuielewa thamani ya Membe.
Wordsworth aliandika kuwa Shujaaa Mwenye Furaha ni yule ambaye kila askari angependa kuwa kama yeye. Roho mkarimu ambaye alifanikisha kila wito wa maisha halisi na kutimiza fikra za wakati akiwa mvulana.
Katika shairi hilo, mistari ya mwishoni, Wordsworth aliandika kuwa Shujaa Mwenye Furaha lazima aizunguke dunia kufanikisha malengo. Na hata kama atakufa pasipo matokeo aliyokusudia, atakuwa mwenye furaha kipindi pumzi yake inakata, huku akipigiwa makofi mbinguni.
Membe tangu uvulana wake alitamani kuutumikia umma wa Tanzania. Kufanikisha viwango vya kutimiza malengo, alisoma Rondo-Chiponda, Rondo mpaka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Haitoshi, alifika hadi Chuo Kikuu cha John Hopkins, Washington DC, Marekani.
Ni mseminari. Ndipo bila shaka alijengwa kimaadili. Baada ya kutoka Rondo-Chiponda na kabla ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Membe alipita Seminari za Namupa, Lindi na Itaga, Tabora.
Akiwa kijana mwenye umri wa miaka 24, tayari alikuwa Ofisi ya Rais, akiwa mchambuzi wa masuala ya usalama wa taifa. Alipokuwa na umri wa miaka 35, taifa lilimtuma Canada, akawa msaidizi wa Balozi wa Tanzania.
Alipofikisha umri wa miaka 46, aliona ni wakati sahihi kuwahudumia wananchi wa jimbo lake. Aliingia kwenye siasa, aligombea ubunge jimbo la Mtama, Lindi, akashinda. Alilihudumia jimbo hilo kwa miaka 15.
Alipokuwa bungeni, kwa nyakati tofauti, taifa kupitia Rais, lilimpa Membe majukumu ya Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani, kisha Nishati na Madini, baadaye akafika utumishi wa juu kabisa katika safari yake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Baada ya tangazo la kifo cha Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, alisema: “Membe alikuwa mtu aliyetosheka. Mara nyingi alipenda kukaa kijijini kwake na kushirikiana na wanakijiji.”
Kwa mujibu wa Mkuchika, mara kwa mara alikuwa akikutana na Membe. Siku zote mwanausalama na mwanadiplomasia huyo aliyebobea, alionesha kuridhika na kila hatua aliyopiga kwenye maisha yake ya utumishi na mavuno aliyopata.
Kwamba hakuwa tajiri ila alitosheka. Na kwa kurejea maneno ya Wordsworth, bila shaka Membe alitabasamu kwa furaha, huku akipigiwa makofi mbinguni. Maana alitosheka na kusudi lililomleta duniani.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tehama, Nape Nnauye, alitoa ushuhuda wake kuwa mwaka 2010, Membe alimwita akagombee ubunge Mtama. Kwa kifupi, Membe alikuwa tayari kumwachia Nape jimbo tangu mwaka 2010.
Kwa mujibu wa Nape, alikataa ‘ofa’ hiyo ya Membe, akachagua kugombea ubunge jimbo la Ubungo, lakini alishindwa kwenye kura za maoni CCM. Kisha, Membe alimwita, akamwambia: “Kugombea Ubungo haukuwa uamuzi sahihi. Mwaka 2015 uje Mtama, sitagombea.”
Kweli, mwaka 2015, Membe hakugombea, badala yake alimshika mkono Nape, mtaa kwa mataa, kata hadi kata, kuhakikisha anashinda. Nape alishinda ubunge Mtama, na hivi sasa anaendelea muhula wa pili.
Ni uthibitisho kuwa Membe alitosheka. Baada ya vipindi viwili vya ubunge, alitaka kuacha jimbo, kilipotimia cha tatu, alistaafu ubunge. Kisha alibaki kuwa mtu mwenye furaha. Nape na Mkuchika wanathibitisha.
Ujumbe unaoupata hapo ni kwamba Membe aliyakadiria maisha yake vema. Ndio maana hakung’ang’ana na ubunge wala vyeo vya uteuzi serikalini. Baada ya uwaziri, alibaki kuwa raia mwenye furaha.
Kwa vile aliyakadiria maisha yake vema, Membe hakuona tabu kuuonesha upande wake wa pili wa kibinadamu, kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli; uanaharakati!
Membe alisimama kama mwanaharakati asiyeogopa kumpa changamoto Magufuli ndani ya CCM, alipoona mambo hayapo sawa. Hata alipofukuzwa uanachama CCM, alihamia ACT-Wazalendo, akagombea urais.
Shabaha kuu ya Membe ilikuwa kumpinga Magufuli, na alisimama hivyo mpaka mwisho. Membe alirejea CCM baada ya hatamu kushikwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Turejee safari ya msibani
Ukishafika Lindi, unahesabu kilometa 55 kufika Rondo. Hicho ndicho kijiji alichozaliwa Membe, alianzia masomo hapo, na pamekuwa nyumbani kwake siku zote za maisha yake. Angezunguka dunia yote, ila mwisho angerejea Rondo.
Angeishi Dar es Salaam na kufanya shughuli zake za siku baada ya siku, lakini maskani kuu ya maisha yake yalikuwa Rondo. Mwisho kabisa, tandiko la usingizi wake wa dawamu limekuwa Rondo.
Ukiwa Lindi unauona msiba wa Membe kwenye macho ya watu. Safari inaendelea hadi kijiji cha Ngongo. Ni umbali wa kilometa 16 kutoka Lindi Mjini. Nyuso za watu zinakiri msiba ni mkubwa kwao.
Kutoka Ngongo hadi Rondo, zinatimia kilometa 39. Hicho ndicho kijiji cha Membe. Maskani kuu ya maisha yake. Wazazi wake waliishi hapo, naye akaendeleza urithi.
Rondo, unakutana na watu ambao nyoyo zao zimepondeka. Bado hawaamini kama kweli Membe ameondoka. Walimwamini na kumtumaini mno. Kwao alikuwa shujaa.
Wananchi wa Rondo wana wasiwasi juu ya maisha yao baada ya kifo cha Membe. Hawaoni na hawadhani kama yupo mwingine ambaye anaweza kuziba pengo lake japo nusu.
Watu wa Rondo watakuonesha alama za Membe kwenye maisha yao. Shule ya Rondo-Chiponda, ambayo alisoma, majengo yake yalikuwa ya tope. Membe aliibomoa na kuijenga upya kwa saruji, imekuwa ya kisasa.
Membe alijenga madarasa ya awali kwenye shule hiyo ili watoto wa Rondo na Chiponda waanze kusoma kuanzia chekechea. Wao hawajui ushiriki wa serikali, daima humwona Membe na juhudi zake binafsi.
Rondo ina soko kubwa la kisasa. Wananchi wa Rondo wanasema lilijengwa na Membe kwa juhudi binafsi, kisha akalikabidhi kwa Halmashauri, ili waliendeshe. Ni soko kiwango cha masoko ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa wana-Rondo, soko hilo, sio tu kwamba limejengwa na Membe, bali pia hata kiwanja ambacho kimetumika ni chake. Vyote hivyo alivitoa kwa Halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya Rondo.
Zahanati ya Rondo, wanakijiji wanaita hospitali. Huwaambii kitu tofauti kuwa serikali ndio ilijenga. Wao wanatoa ushuhuda kwa kujiamini kwamba hospitali yao imejengwa kwa juhudi binafsi za Membe, na hata kiwanja kilichotumika kilikuwa mali yake lakini alijitolea.
Rondo kuna Msikiti mzuri wa kisasa. Waumini wanasali, kisha wanamwombea dua Membe. Msikiti huo ulijengwa na Membe mwenyewe. Majonzi yapo wazi kwa Waislam. Mchango wa Membe kwao hauna kifani.
Sio tu kwa kujenga msikiti, bali ushuhuda unatolewa kwamba kila mwaka, Membe aliwezesha waislamu saba mpaka nane, kwenda kuhiji Makka. Hata mwaka huu, kulikuwa na matajarajio.
Nani mwingine wa kutokea kuziba pengo hilo? Ukiwa msikitini unakutana na mahujaji wa Makka wa miaka tofauti, waliofanikishiwa ibada zao za hija na Membe. Mioyo imepondeka. Membe ameumiza Waislam.
Membe alikuwa Mkristo, tena Mkatoliki, ila hakuwa mdini. Ndio sababu hakuwa na hiyana kusaidia ujenzi wa Msikiti na kupeleka mahujaji Makka. Hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, alitetea waziwazi Tanzania kujiunga na Chama cha Ushirikiano wa Kiislam (OIC).
Mei 15, 2023, mwili wa Membe ukiwasili Rondo. Ratiba ilionesha misa kwa siku hiyo ingefanyika nyumbani kwake. Hata hivyo, Kanisa Katoliki Usharika wa Rondo, uliomba ibada hiyo ifanyikie kanisani kwao, ili kwao iwe misa ya shukurani kwa Membe.
Sababu? Membe ndiye alijenga Kanisa hilo. Uongozi wa Kanisa, ukaona haitakuwa kumtendea haki kama halitaendesha misa maalum ya shukurani kwake. Kifo cha Membe kimegusa madhabahu kanisani hadi mihrab msikitini.
Akina mama na vijana, wanalia kwa namna tofauti. Wapo wanaoguswa kwa jinsi Membe alivyobadili maisha yao, na sasa kawaacha, wengine ni waliokuwa na matarajio chanya kupitia maisha yake lakini amekatika.
Kila mwaka, Membe alikuwa na utaratibu wa kusaidia mitaji ya biashara kwa vikundi vya akina mama na vijana. Hakutaka kumsaidia mmojammoja, aliamini katika vikundi, ili pia wanapojiendeleza inakuwa rahisi kukopesheka.
Membe alidhamini vikundi vingi vya Rondo kupata mikopo benki ili kukuza mitaji yao ya kibiashara na kuzidi kujikwamua kimaisha. Kitendo hiki kilisaidia mno mzunguko wa kifedha Rondo na ukuaji wa kiuchumi. Wananchi wanawaza bila Membe itakuwaje.
Barabara na miundombinu mingi ya kijamii Rondo, kila unapouliza, linatajwa jina la Membe. Kwa kifupi, maisha ya Membe na wana-Rondo yalikuwa na upacha wa hali ya juu, ndio sababu kifo chake kimesababisha giza na upweke mno kila wakiifikiria kesho.