Ghasia zimezuka siku ya Alhamisi katika maeneo tofauti ya mji mkuu wa Senegal, Dakar, baada ya kiongozi wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko, anayetuhumiwa kwa ubakaji, kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa “ufisadi wa vijana”, hukumu ambayo inahatarisha zaidi kuwnia kwake katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024.
Takriban watu tisa waliuawa nchini Senegal katika mapigano kati ya polisi wa kutuliza ghasia na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kufuatia mahakama kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela, wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo ilisema.
Mapigano yalizuka baada ya uamuzi wa Alhamisi, ambao huenda ukamzuia Sonko, mpinzani mkubwa wa Rais Macky Sall, kuwania uchaguzi wa urais mwaka ujao.
Magari na mabasi yalichomwa moto katika mji mkuu wa Dakar na ghasia ziliripotiwa kwingineko, ikiwa ni pamoja na jiji la Ziguinchor, ambako Sonko amekuwa meya tangu 2022.
“Tumeona, kwa masikitiko, ghasia ambazo zimesababisha uharibifu wa mali ya umma na ya kibinafsi na, kwa bahati mbaya, vifo tisa huko Dakar na Ziguinchor,” Waziri wa Mambo ya Ndani Antoine Diome alisema kwenye televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.
Sonko, 48, hakuhudhuria kikao cha kusikilizwa kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo alishtakiwa kwa kumbaka mwanamke ambaye alifanya kazi katika chumba cha masaji mnamo 2021, alipokuwa na umri wa miaka 20, na kutoa vitisho vya kuuawa dhidi yake. Alikanusha makosa na kusema mashtaka hayo yalichochewa kisiasa.
Mahakama ilimuondolea Sonko kwa ubakaji lakini ikampata na hatia ya kosa tofauti lililoelezwa katika kanuni ya adhabu kama tabia mbaya dhidi ya watu walio na umri wa chini ya miaka 21.
Wizara ya sheria ilisema kiongozi huyo wa upinzani sasa anaweza kupelekwa gerezani wakati wowote.
Polisi walisalia kuzunguka nyumba yake huko Dakar huku machafuko yakipamba moto katika mji mkuu na kwingineko baada ya hukumu hiyo.