kurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema Bunge la Tanzania lina haki ya ama kuridhia au kutoridhia mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA).
Mkataba huo ulisainiwa Oktoba 25, mwaka jana kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalumu ya kiuchumi, maegesho ya utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.
Hata hivyo hofu imeibuka kuhusu masilahi ya Taifa kwenye mkataba huo ambapo wanasiasa, wanaharakati na wasomi wanahoji vifungu 31 vya mkataba huo pamoja na nafasi ya Bunge katika kufikia uamuzi wa mwisho.
Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya 1977 kama ilivyorekebishwa, Bunge limepewa mamlaka ya kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
“Kushauri ni moja kati ya kazi za Bunge na zipo nyingine nyingi kwa mujibu wa Katiba, katika hili hapa (mkataba wa IGA) Katiba inasema Bunge ndilo linaridhia kwa hiyo Bunge linaangalia ambacho Serikali imesaini na upande mwingine, basi linaridhia au haliridhii,” amesema Mbossa.
Mbossa ametoa kauli hiyo leo Juni 8, 2023 wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika Kituo cha televisheni cha Clouds 360, asubuhi ikiwa ni mwendelezo wa kutoa ufafanuzi wa hoja na elimu kuhusu makubaliano ya mkataba huo kwa Taifa.
“Kama Bunge halitaridhia mkataba huu hautakuwepo kwa sababu una sharti lazima uridhiwe. Bila kuridhia utatekeleza kwa nguvu ipi?”amehoji Mbossa na kufafanua kuwa maelekezo yoyote ya kurekebisha vifungu vya mkataba huo kutoka bungeni, yatatafsiriwa ni kutoridhiwa kwa mkataba huo.