Ikiwa imebaki siku moja kwa vijana waliomaliza kidato cha sita mwaka huu kuripoti kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zimeelemewa.
Vijana wengi wanakwenda Nida kupatiwa vitambulisho ikiwa ni utekelezaji wa agizo la JKT linalowataka kwenda kambini wakiwa na nyaraka zote zinazohitajika katika usajili wa kujiunga na elimu ya juu.
JKT Mei 25 mwaka huu katika taarifa yake kwa umma iliwataka vijana wote waliomaliza kidato cha sita mwaka 2023, kuripoti katika makambi kwa ajili ya mafunzo kwa mujibu wa sheria kuanzia Juni mosi hadi 11, mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vijana wamejikuta wakikesha kwenye ofisi za Nida na wengine kuwahi alfajiri ili kupata vitambulisho hivyo.
Hata hivyo, Msemaji wa JKT, Meja Janeth Mkamba alisema kutokuwa na namba si kikwazo kwa wanafunzi hao kupokelewa JKT, akisisitiza wanapaswa kuripoti.
“Namba za Nida ni kwa ajili ya maombi ya vyuo, si kwa ajili ya JKT kwa hiyo waje watapokelewa, kutokuwa na namba hakutafanya wakataliwe,” alisema.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na msemaji wa Nida, Geoffrey Tengeneza alisema ili kuharakisha mchakato na kupunguza msongamano, mamlaka ilianzisha usajili kwa njia ya mtandao.
Alieleza usajili huo unafanywa na mwananchi popote alipo kwa kupakia nyaraka zote muhimu mtandaoni, kisha kwenda ofisi za Nida kwa ajili ya hatua za mwisho.
“Tulifanya hivi ili kurahisisha kazi na kupunguza msongamano vituoni, lakini wananchi hawaonekani kutekeleza hilo, wanajazana ofisini.
“Siku zote tunashauri watu wakifikisha umri stahiki wa miaka 18 wajiandikishe kupata vitambulisho, lakini hulka ya Watanzania wanasubiri siku za mwisho ndiyo waamue,” alisema.
Alisema Watanzania wanapaswa kuacha tabia ya kusubiri hatua za mwisho ili kuamua kuhusu jambo lililokuwa na uwezekano wa kumalizwa mapema.
Wilaya ya Ilala
Prisca Mbeda, mkazi wa Kitunda alisema alifika ofisi za Nida wilayani Ilala saa 10 alfajiri ili kuwahi namba na kwamba ni siku ya tatu anafuatilia, ingawa awali alikuwa akifika kwa kuchelewa, hivyo kushindwa kupata huduma.
Akizungumza na Mwananchi jana alisema saa tatu asubuhi alishapata namba, hivyo alikuwa akisubiri kupiga picha na kuchukuliwa alama za vidole.
Naye Azuu Yasin alisema alifika saa 11 asubuhi, lakini alilazimika kusubiri hadi saa 12 ili geti lifunguliwe ndipo aanze kujiandikisha.
Kwa upande wake Maulid Seleman, alisema usumbufu wanaoupata ni baadhi ya wazazi kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, hivyo hutakiwa kuapa kwa mwanasheria ili kupata cheti.
Ofisa Msajili wa Nida Wilaya ya Ilala, John Itimba ameshauri JKT kutoa taarifa mapema za wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na jeshi hilo ili kutoathiri taasisi nyingine katika utoaji huduma.
Itimba alisema muda uliotolewa na JKT ni mfupi ukilinganisha na mchakato wa kupatikana kwa vitambulisho ambao haukamiliki kwa siku moja.
“Kwa wastani na kwa mujibu wa mkataba wetu na wateja walau mwezi mmoja mtu awe amepata namba ya utambulisho tangu amemaliza kuwasilisha na kupitiwa kwa nyaraka zake, ambayo ndiyo sasa inatumiwa zaidi baada ya kusitishwa kutolewa kwa vitambulisho vya kadi,” alisema.
Aliomba iwapo inawezekana JKT iwapokee vijana bila kuwa na utambulisho wa Nida na baadaye wapewe ruhusa ya kufuatilia katika maeneo waliko kwa kuwa Nida ina ofisi katika kila wilaya, ili wasipishane na muda wa kuanza mafunzo.
Itamba alisema kwa sasa wanafanya kazi hadi saa za ziada kutokana na idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja kulinganisha na idadi ya watumishi na vitendea kazi walivyo navyo.
Ili kuepuka kupoteza muda wa kukaa foleni ofisi za Nida, amewashauri wanafunzi, wazazi na walezi kujisajili kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Kupitia mfumo huo, Itimba alisema mhusika akishajaza fomu atakwenda kutoa nakala ya fomu aliyoijaza na kuipeleka Serikali ya mtaa kugongewa muhuri na atakapofika Nida atapigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole tu.
Wilaya ya Temeke
Aisha Juma, mkazi wa Mbagala alisema jana ilikuwa siku ya tatu kufika katika ofisi za Nida na hajafanikiwa kupata kitambulisho.
“Naamka mapema nikifiki hapa napata namba 69, jana (juzi) nilipata namba 56 na ikifika saa 9:30 ofisi wanafunga,” alisema Aisha.
Anania Ngolowe alisema usumbufu mkubwa ni utaratibu wa kuanza upya kupanga foleni siku inayofuata baada ya kushindwa kupata huduma siku iliyopita.
Godfrey Kishapu, mzazi aliyempeleka mtoto wake kupata kitambulisho alisema utaratibu unaotumika si rafiki kwa kuwa muda mwingi wanautumia katika foleni.
“Serikali itusaidie, kama kuna uwezekano wa Nida kuwafuata watoto kambini wafanye hivyo ili kuwasaidia, siku za kuripoti kambini zimebaki chache,” alisema.
Mbeya
Jijini Mbeya baadhi ya vijana wamelalamikia mfumo unaotumika kupata vitambulisho, huku wakitozwa Sh600 kwa ajili ya fomu.
Pia wameonyesha wasiwasi wa kukosa nafasi ya kujiunga na JKT kutokana na kuchelewa muda uliopangwa.
Baadhi yao juzi saa tano usiku walikuwa wamelala eneo la wazi nje ya ofisi za Nida wakisubiri huduma.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Nuru Ally alisema wamekuwa wakifika ofisi za Nida ambako huorodhesha majina, lakini upatikanaji wa vitambulisho umekuwa changamoto.
“Wahudumu walisema wanatoa kwa watu 80 kila siku, sasa kutokana na muda wa kwenda JKT unaisha, tumeamua kuja kukesha hapa ili tusipitwe na huduma, ukisema ulale inakula kwako,” alisema Nuru na kuongeza:
“Fomu tunalipia Sh600, hatujajua inahusu nini, nimetoka nyumbani bila kuaga ili niwahi kuona kama nitapata kitambulisho, tarehe ya kujiunga JKT ni Juni 11 (kesho).” Watumishi wa Nida hawakuwa tayari kuzungumzia sula hilo kwa maelezo kuna utaratibu ambao msemaji ni mkurugenzi mkuu wa Nida, makao makuu.
Hata hivyo, mmoja wa watumishi aliyezunguza kwa sharti la kutotajwa jina alisema wamezidiwa kwa kuwa watu wanaohitaji huduma hiyo ni mengi.
“Ni kweli changamoto hii ipo, sababu kubwa ni vijana kuhitajika kwenda jeshini na muda umekwisha, hivyo tunachokifanya ni kufanya kazi mpaka siku za mapumziko,” alisema.
Imeandikwa Nasra Abdallah, Devotha Kihwelo na Juma Issihaka (Dar es Salaam), Hawa Mathias na Saddam Sadick (Mbeya).