Jumla ya hekari 953 za mashamba ya bangi zimeteketezwa mkoani Arusha katika operesheni iliyofanyika kwa siku nane mkoani humo kuanzia Mei 31 hadi Juni 7, 2023 ikilenga kukabiliana na kilimo cha bangi.
Bangi hizo zimeteketezwa zikiwa bado mbichi shambani ambapo kulingana na makadirio yaliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA) ni sawa na gunia 4,765.
Mbali na bangi hiyo iliyokamatwa shambani ikiwa bado haijavunjwa, zimeteketezwa pia gunia 931 za bangi iliyokaushwa tayari kwa kwenda kuuzwa.
Operesehni hiyo imefanyika ikiwa ni siku chache baada ya kutolewa kwa Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini ambayo imeitaja mikoa inayoongoza kwa kilimo cha bangi huku Arusha ikiwa kinara wa kulima kwa ajili ya biashara nje ya nchi.
Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la kukomesha kilimo cha bangi nchini imeanzia Arusha ambapo kiasi hicho cha bangi kimeteketezwa na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 16.
Amesema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo haya ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa mkoani humo.
“Tumefanya operesheni hii kwa siku nane lakini bado kuna mashamba ya bangi yamebaki, hivyo hii operesheni itakuwa endelevu na pia tunaendelea kutoa elimu ili wakazi wa vijiji hivi waone fursa ya kulima mazao mengine na kuachana kabisa na kilimo cha bangi,” amesema Lyimo.
Baadhi ya wazee wa mila katika jamii zinazolima bangi zimeiomba Serikali kuwapa muda ili waitishe vikao vya wanajamii kuwaelimisha kuhusu hatari ya kilimo hicho na kwa pamoja washirikiane kuyafyeka mashamba yote yaliyosalia.