Mtu mmoja amefariki dunia, huku wengine wanne wakinusurika kifo wakati wakishindana kunywa pombe kali, baada ya kuahidiwa kupewa mkate, sukari na Sh50,000 kwa atakayeshinda.
Tukio hilo limetokea juzi katika kata ya Sanya Juu, wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya watu hao kuahidiwa na mtu anayedaiwa kuwa mfanyabiashara wilayani humo, ambaye sasa ametoroka.
Inadaiwa kuwa mtu huyo aliwaahidi kuwapa zawadi hizo na mpaka mmoja anafariki walikuwa wameshakunywa chupa tano kati ya tisa zilizokuwa zikishindaniwa.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kunywa chupa tano hali zao zilianza kuwa mbaya na wengine kupoteza fahamu ambapo baadaye waliokolewa kwa kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kupata msaada wa dharura.
Mkuu wa wilaya ya Siha, Christopher Timbuka alimtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Benson Mshiri, mkazi wa Kijiji cha Merad na kwamba waliolazwa hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na muda wowote wataruhusiwa kwenda majumbani.
“Uchunguzi wa kidaktari inaonyesha kwamba hiyo pombe inamaliza sukari na maji mwilini na inasababisha kukosekana kwa oksijeni kwenye ubongo.
“Kwa hiyo huyu mmoja aliyefariki ni kutokana na sukari kushuka sana. Maji mwilini yaliisha na oksijeni kwenye ubongo ilikuwa ni kiasi kidogo ndio maana akapoteza maisha,” alisema.
Kuhusu waliolazwa, alisema baada ya kutokea kwa changamoto hiyo waliokolewa na kukimbizwa hospitali ya wilaya, na kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri na muda wowote wanaweza kuruhusiwa.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya mashuhuda walisema watu hao walianza kunywa pombe hiyo kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi jioni, huku baadhi wakiwa hawajala chakula.
Gabriel Munisi, mmoja wa mashuhuda, alisema: “Hawa watu walikuwa wanakunywa pombe kwenye grocery moja hapa Sanya Juu na kuna jamaa alijitolea kuendesha mashindano kwamba atakayemaliza chupa tano atapata zawadi hizo ambazo ni fedha taslimu Sh50,000, mkate na sukari”.
Naye Amos Nkya alisema; “Walianza kunywa pombe muda wa saa sita mchana na ilipofika saa 10 jioni walianza kuanguka kila mmoja kwa wakati wake. Tulianza kuwapepea wengine na waliokuwa na usafiri walisaidia kuchukua wale walioanguka na kuwapeleka hospitali wakiwa hawajitambui.”