KOCHA Mkuu wa Simba, Mbrazil, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameondoka juzi usiku kuelekea kwao kwa ajili ya mapumziko ya msimu baada ya msimu wa Ligi Kuu Bara kufikia tamati, lakini amewaachia majina ya wachezaji ambao hataki kuwa nao msimu ujao ambao leo Simba itayaweka wazi.
Kocha huyo ameondoka na kutoa maagizo mazito ikiwemo ripoti yake usajili ambayo juzi jioni Bodi ya Wakurugenzi ya timu hiyo ilikaa kuijadili kwa mara ya mwisho ikiwemo kupitisha bajeti yake ya usajili mapema.
Championi linafahamu kuwa Mbrazil huyo amewataka mabosi wa timu hiyo kuwa makini katika orodha ya wachezaji ambao anahitaji kuwa nao katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ambayo timu itashiriki.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa Mbrazil huyo aliondoka nchini juzi kuelekea kwao kwa mapumziko huku akiwaachia majina ya wachezaji ambao hawahitaji kwenye kikosi chake cha msimu ujao.
“Ni kweli mwalimu amerejea kwao kwa ajili ya mapumziko lakini uongozi kwa sasa unajipanga kuanza kushusha vitu kwa ajili ya msimu ujao na hii imetokana na kushindwa kufanya vizuri katika michuano yote ambayo tumeshiriki msimu huu.
“Kikubwa ni kwamba ametuachia ripoti yake na nini ambacho anahitaji kwa ajili ya msimu ujao na kesho Jumatatu (leo) tunatarajia kuweza wazi kwa kuwatangaza nyota ambao tumewapa mkono wa kweli msimu huu.”
Hadi sasa Simba imeshatangaza kuachana na kiungo wake mshambuliaji, Mghana, Augustine Okrah ambaye anakuwa ni mchezaji wa kwanza kuachwa na timu hiyo baada ya msimu kumalizika.