KUELEKEA mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Azam FC utakaopigwa leo Jumatatu kwenye Dimba la Mkwakwani Tanga, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ni kama amewaweka mtegoni Azam kwa kuwaaminisha kuwa huenda wachezaji wao watakuwa na uchovu kumbe imefichuka aliamuru mapumziko kabla ya safari ya kwenda Tanga.
Yanga juzi Jumamosi walikuwa na maandamano ya kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambayo yalianzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mpaka makao makuu ya Yanga, mitaa ya Twiga na Jangwani.
Tofauti na msimu uliopita ambapo sherehe za ubingwa wa Yanga zilifanyika mpaka usiku, sherehe za ubingwa juzi Jumamosi zilimalizika majira ya saa 12 jioni ambapo imefichuka ni amri ya kocha mkuu Nabi kwa uongozi ili wachezaji wapate muda wa kupumzika kupunguza uchovu.
Mara baada ya maandamano hayo kikosi cha Yanga jana Jumapili kilisafiri kwa ndege mpaka Tanga kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani humo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nabi alisema: “Tumekuwa na ratiba nyingi katika siku chache zilizopita ambazo kiukweli zimewafanya wachezaji wengi wawe na uchovu mkubwa hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye program za utimamu wa mwili kuelekea mchezo dhidi ya Azam.
“Tunajua ni wapinzani wanaocheza mpira wa maarifa na nguvu nyingi hivyo utakuwa mchezo mgumu sana kwetu.”