KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Safia Jongo amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani hapa inakabiliwa na tatizo kubwa la imani za kishirikina.
Amesema hayo wakati akizungumuza na wakazi wa kijiji cha Kharumwa, kata ya Kharumwa na kueleza kiini cha tatizo hilo ni idadi kubwa ya waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi.
Amesema ramli chonganishi za waganga wa kienyeji zinachangia ongezeko la matukio ya kikatili ikiwemo mauaji ya ndugu ndani ya familia hali inayorudisha nyuma juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama.
“Nyang’hwale tumekuwa na changamoto kubwa ya matukio ya mauaji kwa imani za kishirikina, na imani zenyewe ni uchawi, ambapo mnashika uchawi wazazi wenu, dada zenu eti ni wachawi.
“Mwisho wa siku mnatafuta waganga, na huwa mganga anakudanganya kuna mtu anakata mapanga, mimi nitamuosha atakapokata hatokamatwa, sasa niwaambie serikali na jeshi la polisi tupo macho.”
Amewataka wakazi Nyang’hwale kuunga mkono dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayowekeza katika ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na maji ili kuhakikisha jamii inapiga hatua za kimaendeleo.
“Ndiyo maana rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan anapamabana kujenga mahospitali, anapambana kujenga mashule ili kuwapa watu maarifa, tuondokane na imani potofu, tupate taifa bora.
“Sasa hizi imani za kishirikina tuache mahospitali yapo, sasa hivi kila kata ina hospitali, na sasa hivi kila kata inaongezewa kituo cha afya, kwa hiyo twende kwenye tukatibiwe, tuache imani za kishirikina.”
“Nia ni kujenga taifa lenye maarifa, taifa bora lenye maendeleo, kwa hiyo sisi wazazi tumusaidie mheshimiwa rais kuhakikisha kwamba hawa watoto wanakwenda shule na wanapata elimu bora.”
Kamanda Jongo ameagiza kuundwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi ili kukabiliana na tatizo la matukio ya kikatili ikiwemo ramli chonganishi na kuifanya Nyang’hwale kuwa ya kisasa, bila ukatili na uharifu.