Na Evelyne Ernest
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa, amesema miongoni mwa sababu zinazopelekea wakulima kujiingiza katika biashara ya kuuza mazao yao kwa njia ya magendo ni kutokana na kuuza mazao hayo kwa bei ya juu na kulipwa pesa zao kwa wakati, hivyo kuvitaka vyama vya Ushirika mkoani Kagera, kuhakikisha vinakuwa na bei sawa au zaidi ya ile ya wanunuzi kutoka mataifa jirani huku malipo yakifanyika ndani ya saa 24.
Ameeleza hayo wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya Ushirika na Wadau wa maendeleo ya ushirika mkoani Kagera, katika Uzinduzi wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoani humo, uliofanyika jioni ya Juni 10, mwaka huu, katika Manispaa ya Bukoba, akianza kwa kuvipongeza vyama vya ushirika kwa kazi kubwa ambayo inafanyika ikiwamo ya kuendesha minada ya Kahawa, huku akivitaka kutanua wigo wa bei ya kununua mazao na kuwalipa wakulima fedha yao kwa wakati, kwani kundi hilo halitaki mambo mengi bali kunufaika kutokana na shughuli zao, pia kutumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima kujiunga na vyama hivyo kwani kuna umuhimu mkubwa kimaendeleo na Serikali itaendelea kulinda mipaka ili kudhibiti biashara ya magendo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo, Toba Nguvila amempongeza Mkuu wa Mkoa Fatuma kwa kufanya uzinduzi huo, ambao ni msingi kuelekea katika Siku ya Ushirika duniani, ambapo Kitaifa Maadhimisho yatafanyika mkoani Morogoro, Juni 28 Mwaka huu na Mgeni rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akitaja baadhi yaa changamoto zinazowakabili wakuu wa wilaya kuwa ni pamoja na uwepo wa biashara ya magendo kwani kumekuwapo na siasa nyingi katika ununuaji wa mazao ikiwemo Kahawa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera (KCU) 1990 Limited, Respicious John, amesema sababu kubwa ya kuwapo kwa Jukwaa hilo ni kuthamini mchango wa waanzilishi wa Ushirika, ambao ulielezwa kuanza Mwaka 1940, na miongoni mwa faida ni upatikanaji wa ajira kwa wananchi, kuwasomesha baadhi ya wanakagera, kuanzisha taasisi za kutoa huduma ikiwemo maduka, hoteli na kuchangia huduma za kijamii huku akitaja baadhi ya changamoto kuwa ni matumizi madogo ya TEHAMA katika utoaji wa taarifa kwa wakati, uwezo mdogo wa vyama kukosa mitaji, elimu ndogo ya ushirika na vitabu, watendaji wasio na weledi, upungufu wa wananwake na vijana pamoja na biashara ya megendo, kutozwa kodi na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.