Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)kimempoteza mwanahabari mkongwe, mtetezi wa haki za wanawake na watoto, Leila Sheikh.
Leila ambaye pia amewahi kuwa Mkurugenzi wa TAMWA, kati ya 1996 hadi 2001amefariki ghafla usiku wa kuamkia leo, Juni12, 2023, jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Leila Sheikh atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari na jinsia, tangu kuanzishwa kwa chama hiki, Akiwa mmoja wa waasisi wakeamekuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi mapana ya taifa katika mrengo wa jinsia na haki za wanawake na watoto kiujumla.
Ni miongoni mwa walioshiriki kikamilifu katika mchakato wa kuundwa kwa Sheria ya Makosa ya Jinai, (SOSPA) hadi kupitishwa kwake.
Kabla ya kuwa mkurugenzi wa TAMWA mwaka 1996, Leila alikuwa mhariri wa jarida la kwanza la haki za wanawake Tanzania- Sauti ya Siti mwak 1989, akiwa amedhamiria kupaza sauti kupitia majarida kuhakikisha haki za wanawake zinafanyiwa kazi.
“Aliratibu timu, ambazo zilishawishi Sheria ya Makosa ya Kujamiiana (SOSPA).Katika michakato yote hii, Leila alielewa maadili ya msingi ya mwanaharakati ambayo ni huruma, uelewa, kujitolea, ushirikishwaji, unyenyekevu, ucheshi na amani,”Mkurugenzi wa TAMWA, Dk Rose Reuben.
Leila ni mfano wenye nguvu hasa kwa wakurugenzi wa kike kutokana na kazi aliyoifanya kama mwanamke kijana mwanaharakati, kuendesha shirika, kuhariri jarida la kitaifa na kuongoza mojawapo ya shughuli kubwa za wanaharakati, ambayo iliishia kupata sheria muhimu ya SOSPA.
Alikuwa mwanablog mahiri na atakumbukwa kwa ubunifu wake, hasa baada ya kuanzisha mgahawa wa mtandaoni, aliouita; Leila’s Café, akichambua masuala ya jinsia.
Kwa kuwa alipenda zaidi kutambulika na kutekelezwa kwa haki za jinsia, Leila, alianzisha pia, kundi la facebook, aliloliita Ustawi wa Jamii lililokuwa linajadili masuala ya jinsia pia.
Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe, amemzungumzia Leyla Sheikh na kusema:
“Leila Sheikh alikuwa mwalimu wa wengi kwenye harakati za usawa wa kijinsia na haki za Binadamu. Kupitia TAMWA alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha jamii ya kitanzania inaheshimu na kuthamini usawa kwa watu wote”
Dk Rose Reuben anamzungumzia Leila na kusema: “Leila alikuwa si tu mwandishi mahiri bali pia alikuwa mtetezi wa wanawake aliyetumia taaluma yake ya uandishi”
“Leila Sheikh atakumbukwa kwa ukarimu wake kwa wanahabari, wakati wowote, alipotakiwa kuzungumzia masuala ya jinsia katika vyombo vya habari, alijitoa kwa hali na mali,” Florence Majani
“Pumzika Leila, TAMWA tunakulilia, asante kwa utumishi wako , daima tutaenzi mchango wako.”
Leila alizaliwa 8 Januari, 1958 na amefariki dunia, leo Juni 12, 2023
Amekuwa mwasisi wa TAMWA tangu 1987
Amekuwa mkurugenzi wa TAMWA 1996 hadi Julai 2001
Dk Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji
TAMWA