Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza “Hapa Kazi Tu” umekamilika kwa asilimia 84.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Juni 14, 2023, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL), Eric Hamisi amesema mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh111 bilioni unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi Agosti, mwaka huu.
Amesema tayari Serikali imelipa zaidi ya Sh41 bilioni, sawa na asilimia 31 ya malipo yote kwa mkandarasi Kampuni ya Gas Entec Cooperation inayotekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Gangnam Cooperation na Suma JKT kujenga meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200, tani 400 za mizigo na magari 20.
“Meli tayari imeshushwa majini na ujenzi unaendelea katika hatua zingine. Mkandarasi ameanza kutenganisha vyumba vya abiria ambavyo vinatarajiwa kuwa katika madaraja sita tofauti ikiwemo daraja la VVIP kwa ajili ya viongozi na watu mashuhuri,’’ amesema Erick
Kukamilika kwa meli hiyo kutaongeza shughuli za usafirishaji wa mizigo katika ya mikoa ya Mwanza na Kagera kwa kupunguza usafirishaji kwa njia ya barabara.
Rais Samia Suluhu Hassan amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo huku akimsisitiza mkandarasi na wasimamizi kuhakikisha kazi inakamilika na kukabidhiwa ndani ya muda wa mkataba.
“Nimeridhika na nawapongeza MSCL na timu nzima kwa kazi nzuri, mmeleta kazi na utaalam nyumbani…. tungesema tulifungashe likajengewe huko Korea tusingepata utaalam. Kwa kuijenga meli hii hapa tumepata wataalam tutakaowatumia kujenga meli nyingine,” amesema Rais Samia