Tukio lisilo la kawaida limetokea na kuwaacha wengi midomo wazi baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 76 ambaye madaktari walimtangaza kuwa amefariki dunia, kukutwa akipumua ndani ya jeneza.
Tukio hilo limetokea katika Mji wa Babahoyo nchini Ecuador ambapo inaelezwa kuwa alifikishwa katika Hospitali ya MartÃn Icaza iliyopo kwenye mji huo Ijumaa iliyopita, akiwa amepatwa na shambulio la moyo na kiharusi ambapo alilazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi.
Inazidi kuelezwa kuwa, baada ya madaktari kujaribu kumtibu mwanamke huyo aliyetambuliwa kwa jina la Bella Yolanda Montoya Castro, ilishindikana na akatangazwa kufariki dunia ambapo mwili wake ulikabidhiwa kwa ndugu, kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Gilberto Barbera ni mtoto wa mwanamke huyo ambapo amenukuliwa akisema, alisikia jeneza lenye mwili wa mama yake likigongwagongwa kutokea ndani, ikabidi awaite ndugu wengine na kulifungua ambapo kwa mshangao, walimkuta akiwa hai, anapumua.
Harakaharaka walitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio na baadaye akachukuliwa kwenye ambulance na kukimbizwa kwenye hospitali ileile iliyotoa taarifa kwamba amefariki dunia.
Wizara ya Afya ya Ecuador, imeunda tume maalum kuchunguza tukio hilo na kuahidi kuwa hatua baada ya uchunguzi kukamilika.