Inaelezwa ya kwamba, Marehemu Salma Shaibu enzi za uhai wake alikuwa akiishi na Mumewe Ramadhani Hamisi Wilayani Masasi Mkoani Mtwara.

Taarifa zinaeleza kuwa aliwahi kusafiri na kuelekea wilayani Newala-Mtwara na huko inaaminiwa alishawishika na kuingia kwenye mahusiano na Mwanaume mwingine

Baada ya kurudi nyumbani kwa Mumewe Masasi, Salma hakuwa mwenye furaha na katu hakusimulia kilichomsibu na baada ya kusimulia aliamua kujiua.

Kutokana na fedheha hiyo kumkera moyoni mwake, aliamua kumsimulia rafiki yake wa kike na mdogo wake lakini wote walimpa moyo na kumwambia akae kimya kwani jambo hilo akilisikia mumewe linaweza kuzua balaa. Baada ya kurudi kwa mumewe aliendelea kuonekana mwenye simanzi kubwa, licha ya kuulizwa na mumewe mara kadhaa ni kipi kinamsibu, katu hakumweleza ukweli.

Baadae mumewe bwana Ramadhani aliamua kumuuliza rafiki wa mkewe kwanini mkewe ana huzuni tele, rafiki wa marehemu alimsimulia mume wa Salma yote yaliyojiri baada ya rafiki yake kuchepuka, jambo ambalo halikumshtua mume huyo na kukiri kuwa hilo ni jambo la kawaida na kukiri kuongea na mke wake ili kulimaliza tatizo hilo.

Inasemekana ya kwamba, licha ya Mume kujaribu kumuweka sawa mke wake na kumuambia kuwa hilo ni jambo la kawaida kwani hata yeye kuna wakati hakuwa mwaminifu, marehemu alionekana bado asiye mwenye furaha na ndipo alipoaga kwenda Wilayani Nachingwea kumsalimia baba yake aliyekuwa mgonjwa.

Baada ya kufika Nachingwea, alikaa siku mbili na kuamua kunywa sumu kali ya kuulia wadudu kwenye mikorosho. Taarifa zinasema, Mwili wa Marehemu Salma ulikutwa pamoja na karatasi yenye ujumbe unaosema nimeshindwa kuishi kwa makosa yangu mwenyewe huku mkononi mwake akiwa ameandika ujumbe ambao unaendana sawia na maneno aliyoyaandika kwenye karatasi na kusisitiza sio tatizo la yeyote, bali ni ujinga wake na kujihisi ameikosea familia na Mungu wake.

Baada ya Mwili wa Marehemu kufikishwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mnero, Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi, imebainika ya kuwa alifariki baada ya sumu aliyokunywa kuathiri zaidi viungo vya ndani ya mwili na mfumo wa upumuaji jambo lililosababisha umauti kwa mwanamke huyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Lindi Pili Mande, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa vijana kushirikisha watu mbalimbali masuala yanayowasibu na kupata ushauri namna ya kutatua huku akiwaelekeza kutumia dawati la Jinsia la jeshi hilo kuelezea changamoto mbalimbali za kisaikolojia na mahusiano ili kupata msaada na kuepusha maamuzi magumu ya kujiua.

Marehemu Salma Shaibu, ameacha watoto wawili ambapo mkubwa ameanza kusoma elimu ya awali, Leo tarehe 14 mwezi Juni, amefikishwa kwenye makazi ya milele baada ya kufariki siku ya tarehe 13 mwezi juni mwaka huu.

SUBSCRIBE KWENYE YOUTUBE CHANNEL YETU