Na Evelyne Ernest
HALMASHAURI ya Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera imewataka Wakuu wa Idara na Vitengo kushirikiana kwa pamoja kusimamia miradi ya maendeleo ili iweze kutekelezwa kwa wakati na kwa na ubora unaostahili badala ya kuiachia jamii pekee.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Dokta Peter Nyanja amesema hayo katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi ya Mkurugenzi iliyofanyika ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ambayo imehudhuriwa na wakuu wa idara na Vitengo ameongeza kuwa utendaji wao wa kazi unapimwa kwenye miradi ya maendeleo kwani wapo baadhi ya watumishi hushindwa kusimamia kikamilifu kutokana na kuwepo ubia baina ya mtumishi na fundi wa ujenzi hivyo amewaomba kushirikiana kwa pamoja bila upendeleo ili miradi iwe na tija kwenye jamii.
Naye Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Elias Kayandabila amesema kuwa tayari Halmashauri ilikuwa na mpango wa kuhakikisha jumla ya madiwani 57 ambao bado hawajapata vishikwambi wananunuliwa vishikwambi ambavyo watavitumia katika uendeshaji wa vikao vya Halmashauri ili kuondokana na mfumo wa zamani wa kutumia makabrasha.