Na Nyamiti Alphonce
SERIKALI imesema ina mpango kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya wazee ili kuihakikishia jamii hiyo usalama dhidi ya vitendo vinavyohatarisha maisha yao.
Hayo yameelezwa na Afisa tarafa ya Kahama, mkoani Shinyanga Bw. Juliasi Chagama wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika katika kata ya Ngogwa nje kidogo ya Manispaa ya Kahama.
Bw. Chagama ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama amesema kumekuwa na matukio mengi ya ukatili dhidi ya wazee huku vitendo hivyo vikishamiri kutokana na sehemu kubwa ya jamii kukosa elimu na wazee kushindwa kutetea haki zao kwa kukosa elimu hiyo.
Awali katibu wa Baraza la Wazee wilaya ya Kahama, Mwalimu Anderson Lyimo ameiomba serikali kuanzisha programu za masomo ya uraia na madili ili kuwanusuru wazee na jamii kwa ujumla dhidi ya vitendo vya ukatili.
Naye Afisa wa dawati la Jinsia na watoto wa manispaa hiyo Sajenti Njile Shija amewataka wazazi kukemea vitendo vya ndoa za jinsia moja kwani vitendo hivyo vimekuwa matokeo ya mmomonyoko wa maadili na ukatili.
Tanzania na nchi zingine duniani huadhimisha siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee kila mwaka ikiwa ni takwa mojawapo la uanachama wa Umoja wa Mataifa na haki za binadamu.