Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata 14 Tanzania Bara utakazofanyika Julai 13, mwaka huu.
Kuwepo kwa uchaguzi huo kumetangazwa leo Juni 14, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima ambaye ameeleza kuwa unafanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
“Kwa mujibu wa taratibu, Tume kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, inatoa taarifa kwa Umma kuhusu uwepo wa uchaguzi huo wa madiwani katika kata 14 za Tanzania Bara,” amesema Kailima.
Kailima amezitaja kata hizo kuwa ni Ngoywa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kalola ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui zote za Mkoani Tabora.
Zingine ni Kata ya Sindeni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kwashemshi Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Kata ya Bosha Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga zote za Mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa bosi huyo wa NEC, kata zingine ni Mahege ya Halmashauri ya Kibiti mkoa wa Pwani, Bunamhala ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Njoro na Kalemawe za Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Aidha, uchaguzi huo mdogo pia zitahusu Kata ya Mnavira katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara na Kinyika katika Halmashauri ya Wilaya ya mkoa wa Njombe, Magubike ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na Kata ya Mbede, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi.
Mkurugenzi huyo amesema ratiba ya uchaguzi huo itaanza na utoaji wa fomu za uchaguzi kwa wagombea kuanzia Juni 24 hadi 30 2023, huku uteuzi wa wagombea watakao wania nafasi hizo ukitarajiwa kufanyika Juni 30 mwaka huu.
Kailima amesema kuwa vyama vitakavyopata uteuzi vitaanza kampeni za uchaguzi Julai 1 – 12 mwaka huu na kwamba uchaguzi utafanyika Julai 13, 2023.
“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo katika kipindi cha chaguzi hizi ndogo,” amesema Kailima.