Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Rogatus Mativila kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tamisemi (Miundombinu). Kabla ya uteuzi huo, Mativila ambaye ni Mhandisi kitaaluma alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Zuhura Yunus, imeeleza kuwa, Rais Samia amemteua Mohamed Besta kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads.
Kabla ya uteuzi huo, Besta alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi, Wakala wa Usimamizi wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Cassoa).
Besta ambaye ni pia Mhandisi kitaaluma, ana chukua nafasi ya Mativila ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi.
Utezi mwingine alioufanya Rais Samia ni wa Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kamishna Wakulyamba amechukua nafasi ya Anderson Mutatembwa ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), anakoenda kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amemteua Amin Nathaniel Mcharo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Tanroads.
Taarifa hiyo inaendelea kueleza kuwa teuzi zote zimeanza toka Juni 12, 2023.
Katika tukio jingine, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka, kuwa na Hadhi ya Balozi. Katika uteuzi huo, pia amewateua Dk Salim Othman Hamad, na Dk Kassim Mohamed Hamis kuwa na hadhi hiyo ya Balozi.
Wakati Dk Hamad ni Msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya Siasa, Dk Khamis ni Msaidizi wa Rais anayeshughulikia Hotuba.
Aidha, taarifa ya Ikulu inaonyesha kuwa hadhi hiyo ya Ubalozi inaenda sambamba na vyeo walivyo navyo na kwamba uteuzi umeanza toka Juni 12, 2023 japo wataapishwa Juni 16 mwaka huu.
Katika tukio jingine, Rais Samia viongozi wanasiasa wanne kuwa Washauri wa Rais – Siasa na Uhusiano wa Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari, imewataja Wanasiasa hao kuwa ni William Lukuvi, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa.
Wengine ni Abdallah Bulembo ambaye ni Mbunge mstaafu, Balozi Rajab Omar Luhwavi ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji na Haji Omar Kheir ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri mstaafu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, imesema uteuzi wao umeanza Juni 13, 2023.