Mahakama Kuu imeamuru kurejeshwa chuoni mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya sheria ya Chuo Kikuu Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Mwajuma Malulu aliyefukuzwa kwa madai ya kukiuka kanuni za mitihani.
Katika uamuzi alioutoa juzi na nakala kupatikana katika mtandao wa Mahakama Kuu jana, Jaji Abdi Kagomba aliamuru kufutwa kwa uamuzi wa Tudarco wa Septemba 21, 2022 wa kumfukuza chuo mwanafunzi huyo.
Mbali na uamuzi huo, Jaji Kagomba alitoa amri kwa Tudarco kumruhusu mleta maombi kufanya mitihani yake ya majaribio ya muhula wa pili kama alivyoomba kwa kuwa hakuifanya.
“Inavyoonekana mleta maombi alifukuzwa na seneti. Ninaona hivyo kwa sababu kamati ya taaluma ya chuo ndiyo ilichunguza tukio hilo na kutoa mapendekezo yake kwa seneti, kwa hiyo uamuzi wa mwisho kumfukuza ulikuwa ni wa seneti,” alisema Jaji.
“Kama ndivyo hivyo, mleta maombi alitakiwa akate rufaa chombo gani kingine cha juu kama hakuridhika na uamuzi wa seneti?” alihoji Jaji.
Pia, alisema kwa utaratibu wa chuo, kama angekata rufaa, bado ingesikilizwa tena na seneti.
Julai 21, 2022, Malulu, aliyekuwa mwaka wa mwisho, aliandikiwa barua na chuo, akitakiwa kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua kwa kukiuka kanuni za mitihani, ikidaiwa alifanyiwa mtihani wa majaribio na mwanafunzi mwenzake.
Malulu aliwasilisha maelezo akikanusha kumruhusu mtu yeyote kumfanyia mtihani na akamtaka mwanafunzi aliyedaiwa kumfanyia mtihani huo, Bahati Mfaume naye kumpa maelezo. Mfaume alidai kuwa alimfanyia Malulu mtihani huo kwa kumuonea huruma kwa kuwa kulikuwa na ratiba ya mtihani na alikuwa nje ya chuo.
Alidai kuwa Malulu alikuwa hapatikani kwenye simu kwa kuwa alikuwa akimhudumia mtoto wake mchanga.
Mwanafunzi huyo (Mfaume) kwa unyenyekevu aliomba msamaha na kuahidi kutorudia kitendo hicho, lakini seneti ya chuo ilibariki mapendekezo ya kamati ya taaluma kwamba Malulu ana hatia ya kosa hilo.
Septemba 26, 2022 Malulu aliwasilisha ombi kwa mujibu maombi ambaye ni Tudarco, kufanya marejeo ya uamuzi wake huo akiegemea uzito wa utetezi wake, ushahidi wa mdomo na ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu za Tudarco.
Pia, akaijulisha Tudarco kuwa angefungua maombi mahakamani kama ombi lake la marejeo ya uamuzi wao lisingefanyiwa kazi kwa wakati na kumpa nafasi ya yeye kuhitimu mafunzo yake, lakini hakuwahi kupata majibu.
Kutokana na hali hiyo akafungua maombi ili Mahakama itoe amri kwa Tudarco kufuta uamuzi wake na kumrejesha chuoni kama mwanafunzi .