Rais Samia Suluhu Hassan amesema utendaji mzuri wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara nchini (Tanroads) Rogatus Mativila ndio sababu ya kumpandisha kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi – Miundombinu.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 16, 2023 Ikulu jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi watano aliowateua hivi karibuni.
“Bado tunacheza drafti la kupanga Serikali na ndivyo inatakiwa kwasababu maendeleon ni ‘adjustment’ ukiona mambo yanakwama hapa ‘unaadjust’ hapa mpaka upate laini sawa sawa katika kila sekta
“Nimefanya teuzi hizi ndogo, Tamisemi nimemteua Mativila alifanya kazi nzuri sana akiwa Tanroads nikaona nimpandishe awe Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Miundombinu), Tamisemi ni dude kubwa sana lakini watu ni wachache hivyo Mativila atatusaidia hapo,”amesema.
Rais Samia amesema katika wizara hiyo yenye waziri, naibu waziri katibu mkuu na manaibu wake hawajaenea hivyo amemuweka Mativila ambaye atakwenda kushughulikia miundombinu peke yake lakini pia atahusika na kuwasimia wakuu wa mikoa.
Aidha, amesema ndani ya Tamisemi kuna Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) na hata Tanroads wanafanya kazi na Tamisemi hivyo lazima awepo mtu atakayekwenda kusimamia miundombinu yote inayojengwa ikiwemo shule na vituo vya afya na barabara vijijini.
“Lazima tuwe na mtu wa miundombinu hivyo nikahisi Mativila anatufaa kwenda kusimamia miundombinu yote inayojengwa nchini nzima kwa thamani ya fedha zinazotolewa,” amesema.