Serikali wilayani Kiteto imepiga marufuku wananchi kukodi mashamba bila kushirikisha uongozi wa Kijiji hali inayodaiwa kuwa ndio chanzo cha migogoro ya ardhi wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mbaraka Batenga ameyasema hayo leo Jumapili Juni 25, 2023 mbele ya wakulima, wafugaji, viongozi wa dini na wafanya biashara mjini Kibaya katika kikao maalum.
“Ni marufuku mtu kukodi shamba bila kushirikisha uongozi wa Kijiji husika…kwa sababu watu wanakodi maeneo ya malisho na kulima kisha baadaye inaibuka mgogoro isiyo ya lazima,”amesema
Amesema asilimia 60 ya muda wake anatumia kutatua migogoro ya ardhi zaidi kuliko shughuli nyingine za maendeleo, huku akidai lengo la uwepo wake hapo ni kuhakikisha jamii inapata maendeleo
“Sasa kwa Kiteto ni tofauti na maeneo mengine, hapa natumia asilimia 60 kufanya kazi ya kutatua migogoro ya ardhi zaidi kuliko shughuli zingine za maendeleo jambo ambalo sio wanalolitaka wananchi wao wanataka maendeleo,”amesema.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kiteto, ACP George Katabazi katika kikao hicho kilicholenga kuondoa changamoto ya ardhi amesema kiongozi yoyote atakaye bainika kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi asifumbiwe macho
“Jamani kama mtaona kiongozi yoyote kuwa ndio chanzo cha migigoro ya ardhi tusimfumbie macho,” amesema ACP Katabazi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Ngarenaro, Abubakari Kidevu amesema ili migogoro ya ardhi Kiteto iweze kuisha ni lazima viongozi wa mila wawe wakweli kusaidia Serikali na jamii na kuacha kuogopa mila kuliko Serikali.
Katibu wa Chama cha Wafugaji Kiteto, Tipis Masiaya amesema tatizo mifugo hivyo kusababisha kukosekana eneo la kuchunga.
Hata hivyo kikao hicho kimeazimia Desemba mwishoni kuwe na kikao cha pamoja tena Jeshi la Polisi na wadau hao kuangazia utekelezaji wa maazimio hayo.